Monday, April 25, 2011

SHEREHE ZA MUUNGANO MARA HII NI HAPA

Makamu wa pili wa rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akitoa taarifa kwa kamati ya sherehe na mapambano kuhusu sherehe za Muungano kufanyika hapa Zanzibar, kulia kwake ni Katibu Mkuu Khalid Mohammed na kushoto ni waziri wake Mohammed Aboud Mohammed
Sherehe za kuadhimisha miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinatarajiwa kufanyika rasmi hapa Zanzibar tarehe 26 April, 2011 katika Kiwanja cha Aman Mjini Unguja.Taarifa hiyo rasmi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Zanzibar, ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Balozi Seif Ali Iddi katika kikao cha Halmashauri hio kilichofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi wa Mnazi Mmoja.
Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshatoa uwamuzi huo ambao umepokelewa kwa furaha na tayari umesharidhiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dr Ali Mohd Shein.
Kikao cha leo kilikuwa na Madhumuni ya kupokea taarifa hiyo na mapendekezo ya Kamati Tendaji ya Maandalizi ya Sherehe hizo, yaliyotokana na mikutano miwili ya Kamati Tendaji zilizokua na wajumbe wa Bara na Visiwani iliyofanyika Zanzibar na Dar es Salaam katika miezi ya Februari na March mwaka huu.
Wakati huo huo Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameliagiza Baraza la Manispaa la Mji wa Zanzibar kuweka taratibu nzuri za utupaji wa taka katika Mji huo na kuwaelimisha wananchi wasitupe taka ovyo.
Agizo hilo alilitoa katika ziara fupi aliyoifanya katika pwani ya Kilimani na Bustani ya miti mashuhuri ya Kilimani juu, kuangalia hali ya usafi katika maeneo hayo kwa wakati huu wa mvua za masika.
Aidha, alikubali ushauri wa Mwanachi mmoja Ndugu Issa Mohammed wa kuzuwia mmongunyuko wa ardhi kwa vigogo vya minazi katika eneo la pwani ya Kilimani ili maji yasipande juu mitaani.

No comments:

Post a Comment