Thursday, April 28, 2011

UDUGU NA MWANA-NYIKAA


                                                                                                                              

                                                                                

Udugu tulionao, si wa damu si nasabu
Si wa ndewe si sikio, si jamaa si karabu
Udugu masingizio, kuzidiana hesabu
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda

Mwananyika eniona , ‘mekaa nimetulia
Bukheri mwana mwanana, usoni naendelea
Akajifanya yu mwema, “ati” anisaidia
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda

Si kwamba neukubali, udugu na Mwananyika
Nejua he’mtu bali, ulikuwa ni mzuka
Wetumwa ni majangili, kuja nitia wahaka
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda

Udugu udugu gani, yeye pima miye nyanda?
Udugu uso mizani, yuanenepa nakonda
Nikikwama mijibani, yeye mbele yuasonga
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda

Udugu udugu gani, udugu wa kunyonyana
Mwananyika maluuni, nachuma yuakusanya
Sina kitu mfukoni, kwake i tele hazina
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda

Udugu udugu upi, bila ya misingi yake
Haki yangu siipati, changu chake chake chake
‘mefika sasa wakati, kila mmoja kivyake
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda

Nshachoka nshachoka, zigo hili mabegani
Udugu nawe hakika, ushafika ukingoni
Katangetange na nyika, zinga wapya wahisani
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda

Siutaki ukhiwani, usiokuwa na kheri
Nauvua kwa Yasini, Jowsheni na Ha’badiri
Saba w’arbaini sinina, ‘shastahmili
Udugu nawe hakika, siuwezi umenishinda!

1 comment:

  1. What type of books did they give me in history class ? ? ? Or was that a way to cover-up and intend to keep us stupid ...... for how long?

    ReplyDelete