Thursday, April 28, 2011

WANASIASA WASHAIGIWA NA WASI WASI THAIDI YA MUUNGANO

WAKATI Tanzania leo ikiadhimisha miaka 47 ya Muungano, baadhi ya wanasiasa nchini wameonyesha wasiwasi kuhusu hatima yake na kutaka mjadala wa Katiba unaoendelea nchini, utumike kuunusuru.Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana wanasiasa hao walisema, kuna kila dalili za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuvunjika muda mfupi ujao kama hakutakuwa na mkakati maalumu wa kuunusuru.
Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombare Mwiru amewataka Watanzania kuuenzi Muungano kwa kuendeleza umoja na amani katika jamii: “Tanzania ni moja na sisi (Watanzania) ni wamoja, hakuna haja ya kulumbana kiasi cha kugawanyika katika kipindi hiki ambacho mataifa mengi yanataka kuungana.
“Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mjadala wa Katiba unaoendelea sasa nchini, unapaswa pia utumike kujadili muundo mpya wa muungano ambao utaondoa malalamiko.“Watu wapewe uhuru wa kujadili muundo wa Muungano wao ili kuondokana na kasoro ambazo zimekuwa zikilalamikiwa, hiyo itasaidia kuwa na Muungano imara zaidi,” alisema Mbatia.
Kwa mujibu wa Mbatia, Muungano ni kitu adhimu na si vyema kuzungumzia kuuvunja katika kipindi hiki ambacho nchi nyingi duniani, zinataka kuungana ili kuwa na nguvu ya pamoja.“Kwa kweli nitamshangaa mtu anayezungumzia kuvunja muungano katika kipindi hiki ambacho mataifa mengi duniani, yanafikiria kuungana.
Jambo la msingi hapa ni kuumarisha kwa kuondoa kasoro zilizopo,” alisema.Mbatia alisema hilo litawezekana ikiwa watu watapewa uhuru wa kujadili masuala mbalimbali yanayouhatarisha.Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni silaha kubwa katika mapambano dhidi ya umaskini.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na viashiria vinavyohatarisha uwapo wake na kusema busara inatakiwa kutumika ili kuunusuru.Mrema alisema moja ya viashiria vya kuvunjika kwa Muungano ni kauli za hivi karibuni kuhusu Muswada wa Katiba kwamba Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein hakushirikishwa kuuandaa.
“Wanasahau kwamba Rais Kikwete ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyechaguliwa na Watanzania wote, wakiwamo Wazanzibari,” alisema Mrema na kuongeza:“Kwa hiyo hizi ni kasoro zinazoashiria kuvunjika kwa muungano kama hazitadhibitiwa. Tunahitaji mazungumzo ili kujadili kero zinazolalamikiwa.” Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei alisema Muungano wa kulazimishana hauwezi kuwaletea matunda Watanzania.
“Wazanzibari wanaona kama vile tunawalazimisha katika Muungano. Wanaona kwamba watu wa bara ndiyo wanaofaidika zaidi nao.
Katika majadiliano ya Katiba mpya, Muungano ujadiliwe kwa uwazi ili kama Wazanzibari hawautaki tuuvunje, tusilazimishane, vinginevyo kila siku tutakuwa katika matatizo.”Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwataka wananchi kuzungumzia pia mambo mazuri yaliyopo kwenye Muungano badala ya kujadili yaliyo mabaya pekee.
Alisema kwa kuzungumza mambo mabaya pekee, kunawafanya vijana na watoto kukua wakiwa na dhana kuwa, Muungano hauna jambo lolote jema.“Tujivunie mengi mema yaliyo kwenye Muungano kuliko kutumia muda mwingi kila tunapokutana kuzungumzia mabaya tu.
Mazuri ya Muungano pia, yazungumzwe,” alisema Nape.Alisema Watanzania wanatakiwa kuadhimisha miaka 47 ya Muungano kwa furaha na kujiamini kwa kuwa mbali na kuwa ni Muungano wa muda mrefu, umewaunganisha Watanzania na kudumisha upendo miongoni mwao.

No comments:

Post a Comment