Tuesday, May 1, 2012

WAZENJI WAFURIKA VIWANJA VYA LUMUMBA(MUUNGANO USIO NA RIDHA NI JINAMIZI LISILO KUBADUKA)


Mwanasheria Maarufu Zanzibar, Salum Tawfiq akitoa mada katika Kongamano la Kitaifa kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika viwanja vya Lumumba Mjini Zanzibar
Wazanzibari waliofurika katika viwanja vya Lumumba katika kongamano lililozungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo watu kadhaa walitoa uzoefu wao wa maisha ndani ya Muungano

Mimi naamini kabisa kwamba Muungano ni ridhaa baina ya Nchi mbili zilizoungana. Muungano wa Serikali mbili au viongozi wawili bila ya baraka za watu wa nchi hizo hauna maana yoyote. Hivyo iwapo upande mmoja katika Muungano utasita kuridhia kubaki katika Muungano, huo unakuwa si Muungano tena. Sasa leo ya nini kuunda Tume na kupoteza mabilioni ya fedha kujaribu kuutenganeza upya Muungano ambao tayari viashiria vyote vinaonesha Muungano ushapitwa na wakati. Si ungetosha tu kuwauliza Watanzania suala la msingi kwanza kabla ya kuingia katika gharama zisizo za lazima. Suala lenyewe: jee unautaka au huutaki? Kungekuwa na haja gani ya kutaka Muungano uwe madhubuti kama walio wengi hawautaki?
UTATUZI WA KUDUMU WA KERO ZA MUUNGANO
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao juzi tu ulitimiza miaka 48 umejaa kero ambazo kila upande, hasa Zanzibar, unaona zimekua karaha. Muungano huu na kero zimekuwa ni vitu vinavyokwenda pamoja – huwezi kuzungumzia Muungano bila ya kuanza kutaja mapungufu yake. Katika mada hii, nitajaribu kupendekeza namna ambavyo kero hizi tunaweza kuzitatua.Mwalimu Nyerere akihojiwa na Gazeti la Observer la Uingereza tarehe 18 Aprili 1968 alisema:Kama ni Rais wa Tanzania, ni jukumu langu kulinda kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano. Lakini iwapo umma wa Wazanzibari, bila ya kutumiwa na wageni, wakiwa na sababu zao binafsi, wakaona kuwa Muungano hauna maslahi kwao, sitoweza kuwalazimisha kubaki katika Muungano. Muungano utakuwa tayari umesita kuwepo endapo upande mmoja utaondoa ridhaa yake. (Tafsiri ni yangu).Nukuu hiyo ndio chimbuko la mada yangu. Katika harakati au wasemavyo siku hizi “mchakato” wa kupitishwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, Wazanzibari wameonesha wazi kwamba wamechoshwa na Muungano uliopo sasa. Wazanzibari walio wengi pamoja na viongozi wao, wakiwemo Mawaziri na viongozi wa dini, wamesema waziwazi kwamba Muungano huu wa miaka 48 hauna maslahi kwao. Na “Baba wa Taifa” alishaota ndoto hio; leo kero za Muungano zinaonekana zaidi kwa ndugu mdogo (Small Brother) kuliko kwa kaka mkubwa (Big Brother).Wapo baadhi ya Watanganyika ambao nao wamekuwa wakidai Tanganyika yao lakini hawa ni katika wachache. Waliowengi, kuwepo au kutokuwepo kwa Zanzibar katika Muungano hakuathiri chochote kwao. Hawa wanaona ukubwa wa ardhi, idadi ya watu na rasilmali nyingi walonazo zinaitoa Zanzibar kama mshiriki mwenza (equal partner) katika Muungano. Hili likichanganyika na “kero ya Wazanzibari” kila siku kufanya kelele linawafanya waone Muungano hauna maana tena kwa Tanzania.Wapo Watanganyika wengine wanaona Zanzibar “haina shukrani” kwa kuwa ati Zanzibar inategemea kila kitu – kuanzia chakula, nguvu kazi na hata fedha za kuendeshea nchi kutoka Bara. Hawa ndio wengi wanaosema Muungano unawanufaisha zaidi Wazanzibari na itakuwa ni kujitia kitanzi iwapo Zanzibar itajitowa katika Muungano.
Tabaan. Kwa wote hawa basi na warudi wenyewe kwa Mwalimu Nyerere. Sasa Zanzibar na Wazanzibari washaridhika kwamba Muungano umewachosha. Kuna haja gani ya kuunda Tume ya Katiba kukusanya maoni ya wananchi?Sheria ya kuanzisha Tume ya Katiba imeweka hadidu za rejea au muongozo kwa Tume hiyo ambayo inategemewa kuanza rasmi kazi yake mwanzo wa mwezi wa Mei, 2012. Hadidu rejea hizi zimetajwa katika kifungu cha 8, 9 na 17 vya Sheria hiyo (Nam. 8 ya 2011). Baadhi ya majukumu yake ni:
Kukusanya maoni ya wananchi Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu rejea
Kutayarisha na kuwasilisha ripoti kwa kuzingatia hadidu rejea. Agenda kubwa kwa Wazanzibari ambayo ni suala la kuwepo au kutokuwepo kwa Muungano si miongoni mwa hadidu rejea za Tume ya Katiba. Na wakati wa kuapishwa kwa Wajumbe wa Tume Ikulu Dar es Salaam tarehe 13 Aprili 2012, Rais Kikwete alisema wazi kwamba wanaohubiri kuvunjika kwa Muungano hawatasikilizwa! Mtu ataweza kujiuliza: nini sasa faida ya kukusanya maoni kama kiini cha matatizo hutaki kijadiliwe? Katika kulijadili hili naomba tukakisome tena kitabu cha Baraza la Katiba, Zanzibar:Katiba Tuitakayo – Sheria ya Kuandika Katiba Mpya ya Tanzania na Suala la Muungano kwa Zanzibar, hususan Sura ya Nne (Uk.22 – 29).
Maana yake ni kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Tume, hata kama Wazanzibari asilimia 100 wakisema wamechoshwa na Muungano hawatasikilizwa! Hapa ndio udhaifu mkubwa wa Sheria ya Tume unapoonekana. Nini hasa faida ya kuunda Tume na kutumia zaidi ya bilioni 40 na kumalizia kwa kuongeza tu katika orodha ya kero za Muungano?Napenda hapa niunganishe hili la kuundwa kwa Tume ya Katiba na kupitishwa kwa Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar (Sheria Nam. 9/2010). Marekebisho haya yameingiza vifungu vingi ambavyo kwa maumbile yake vinaonekana vikisisitiza Utaifa (Nationhood) wa Zanzibar. Kifungu cha 1 kinasema:Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.Kifungu cha 2A nacho kimetowa mamlaka kwa Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo. Pia viko vifungu vyengine vinavyoonesha dhahir kujibu kejeli ya kaka zetu wakubwa kwamba Zanzibar ni mkoa tu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunafahamu jinsi mara kadhaa wanasiasa wa Tanzania Bara na hata Mahkama ya juu kabisa ya Tanzania (Mahkama ya Rufaa) walivyosisitiza kwamba Zanzibar si Nchi. Kwa maana hiyo hata ukifanya njama ya kutaka kumuondoa Rais wa Zanzibar madarakani kwa mtutu wa bunduki, hiyo haitokuwa uhaini (treason).Ni sawa sawa na kujaribu kuiondosha Halmashauri ya Mji wa Chake Chake, si jambo la kushtua!Mimi naamini kabisa kitendo cha Baraza la Wawakilishi kupitisha Marekebisho hayo kimekuja katika wakati muwafaka kabisa. Unapokuwa na mwenzako ambae hafahamu lugha unayozungumza inabidi utafute lugha pekee atakayoifahamu. Kubadilisha Katiba imekuwa lugha muwafaka kuwafanya wenzetu waone nini tunataka. Marekebisho ya Katiba yameibua lawama tele kutoka kwa wanasiasa na hata miongoni mwa wanasheria mahiri wa Tanzania Bara. Wengine wamesema Muungano wa Tanzania haupo tena pale Zanzibar ilipojitangaza kuwa ni Nchi! Mie naziona hizi zote ni kelele za mlango tu.Kwa upande mwengine naamini Marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya 2010 pamoja na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ndiko kulikopelekea kaka zetu wakubwa kuleta kiini macho cha Tume ya Katiba. Kama kweli lengo la Tume ni kushughulikia kero za Muungano na kuufanya Muungano wetu kuwa madhubuti basi hilo lilipaswa kufanywa zamani sana, pale kelele za Wazanzibari na hata za makundi kama G 55 ya Tanzania Bara yalipoibuka kudai Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar.
Badala yake hali ya kisiasa ikawachwa kuwa tete. Waliokosoa Muungano wakaitwa wasaliti wasioitakia mema Tanzania. Kuunda Tume ya Katiba sasa hivi ni sawa na kujaribu kuyazuia maji ya bahari yasifike ufukweni wakati wa bamvua!Suala la kuwepo au kutukuwepo kwa Muungano ndio suala la msingi hata kabla ya kuunda Tume. Hapa Zanzibar tunayo Sheria ya Kura ya Maoni, 2010. Bara hawana, lakini hilo haliathiri chochote. Kama alivyonukuliwa Nyerere mwanzoni mwa mada hii;Muungano hauwezi kuwepo endapo upande mmoja utaukutaa. Cha msingi ni kulipeleka suala hili kwa wananchi wenyewe walitolee uamuzi. Kwani viongozi wanahofu ya kitu gani? Isije ikatufika hadithi ya Abunuwasi ya kuwekwa uchi halafu tukaamini hatuonekani!Mimi naamini kabisa kwamba Muungano ni ridhaa baina ya Nchi mbili zilizoungana. Muungano wa Serikali mbili au viongozi wawili bila ya baraka za watu wa nchi hizo hauna maana yoyote. Hivyo iwapo upande mmoja katika Muungano utasita kuridhia kubaki katika Muungano, huo unakuwa si Muungano tena. Sasa leo ya nini kuunda Tume na kupoteza mabilioni ya fedha kujaribu kuutenganeza upya Muungano ambao tayari viashiria vyote vinaonesha Muungano ushapitwa na wakati. Si ungetosha tu kuwauliza Watanzania suala la msingi kwanza kabla ya kuingia katika gharama zisizo za lazima. Suala lenyewe: jee unautaka au huutaki? Kungekuwa na haja gani ya kutaka Muungano uwe madhubuti kama walio wengi hawautaki?Kwa mawazo yangu endapo Wazanzibari watasema hawautaki Muungano, dawa iliyobaki ni moja tu nayo ni kumaliza taratibu mambo ya Muungano. Udugu wa watu wetu na mahusiano ya kidiplomasia yatandelea. Marehemu Karume aliunasibisha Muungano na koti: likikubana utalivua tu. Nadhani koti la Muungano limekuwa linawabana sana Wazanzibari na lililobaki ni kulivua tu. Tukingoja sana itabidi tulichane kwani litashindwa kuvuka!
Ahsanteni Sana
Imetayarishwa na:
Salum Toufiq, Wakili
(Mada iliyotolewa katika Kongomano lililofanyika Lumumba tarehe 01 Mei 2012)

No comments:

Post a Comment