Tuesday, July 10, 2012

KWAHERI MUUNGANO WA THAARUBA NA MATESO KARIBU ZANZIBAR MPYA YANYE KHERI NA BARAKA

Nianze kwa kukopi kianzio cha kitabu cha msomi wa Kizanzibari Dk Harith Ghassany alipoandika, “Na mtaujua ukweli na ukweli utawaweka huru – Biblia Yohane 8:32” na uchokozi wa makusudi ninaoulekeza upande wake kwamba wakati umefika wa muendelezo wa kitabu chake cha ‘ Kwaheri ukoloni, kwaheri uhuru! ,’ kwa kuingia mzigoni kuikaribisha Dola adhimu ya Zanzibar kwa kuizika ile iliyoikifikirika. Na jina nampendekezea hilo hapo juu!
Uchokozi huu si wa shari, bali wa kheri kabisa, wenye lengo la kusonga mbele katika malengo yetu ya Zanzibar iliyo huru – bila ya kusubiria maamuzi ya wanaosita sita kuusubiria upande wa pili wa muungano uamue, maamuzi ni yetu sisi Wazanzibari na hayawahusu watu wa upande wa Tanganyika.
Tunashuhudia katika dunia ya leo ya mabadiliko ya kasi katika njanja zote kuanzia jamii na teknolojia kwamba si wakati tena wa mwananchi kubaki nyuma akisubiri maamuzi ya wachache walio juu katika ngazi ya uongozi, bali ni mwananchi mwenyewe aliye na jukumu la kumuongoza pia kumshauri anaemuongoza kwa kumuelezea ni kipi anachokitarajia kutoka kwake.
Matakwa na matarajio ya Wazanzibari walio wengi ni kuona Dola huru ya Zanzibar yenye mamlaka kamili katika ulimwengu huu inasimama; hawaitaki nchi tegemezi inayosubiria amri ama kujibu amri kutoka upande wowote ule ila kutoka kwa Wazanzibari tu.
Mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania (binafsi naiita ya Tanganyika – maana sioni wao wanaongozwa na ipi), kwa upande wangu naufananisha na mgawanyo wa yaliobaki katika madaraka ya Zanzibar yaliyomo ndani ya katiba hio; yaliyomo yanayohusu Zanzibar yatolewe na kuyakabidhi madaraka hayo kwa wenyewe halali, nao ni Wazanzibari wanaowakilishwa Uzanzibari wao kupitia katiba ya Zanzibar.
Hatuna muda tena wa malumbano na mabishano na wabia wa muungano huu, wametaka kuamka na kulirudisha jina lao la Tanganyika iliyojificha nyuma ya jina la Tanzania ni sawa – la hawataki hio ni shauri yao, ningeliwashauri kwamba wakati wa kufanya hivyo ni sasa kupitia mchakato wa katoa maoni kupitia katiba hii. Kwa mujibu wa Warioba maoni ya kuhusu muungano yatashughulikiwa, na muungano huu ninaoufahamu mimi ni kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Mh Tundu Lissu amewafahamisha vyema katika hotuba yake bungeni, nimkumbushe pia awashajiishe Wana Chadema kudai hilo ikiwa kweli ana nia ya kuiona nchi yenye jina la Tanganyika inarudi; daini jina lenu na mamlaka yenu yarudi. Nasi tuna yetu yanayotushughulisha yatayohitaji usimamizi imara.
Ni wakati muafaka wa Zanzibar kuanza kufikiria vyema ni kipi cha muungano tulichokichanganya tugawane na yale yote yalioengezwa kinyume na makubaliano ya awali baina ya waasisi wawili kurudishwa kwa wenyewe halali. Na pia kufikiria namna gani rasilimali za Zanzibar zitatumika ipasavyo katika kuinua hali za Wazanzibari kiuchumi na ustawi wa jamii yake.
Ni wakati wa mipango na mikakati kabambe ya kuepukana na kuja kufeli kwetu tutapopata nchi yetu kamili. Hatutegemei kwa mfano rasilimali yetu ya mafuta kuja kua ni nuksi baada ya manufaa kwetu kama ilivyo Nigeria. Nigeria licha ya kuwa na mafuta ya kutosha walichofaidika ni vita na uharibifu wa mazingira huku wachache tu wakijifaidia matunda ya rasilimali hiyo. Na manufaa ya wingi wake yakielekea nchi za Magharibi zenye kumiliki makampuni nchini humo, ambao ndio wachafuzi wakuu wa mazingira ya nchi hiyo.
Naelewa katika uandishi huu kuna baadhi yetu wataona kwamba naanza kuota ndoto za alinacha, ila jawabu langu ni kwamba hakuna kinachoanza chochote bila kwanza kukiota/kukifikiria. Tusonge mbele kwa kuwapa msukumo huu viongozi wetu, tunachokitaka kiwe ndio matokeo, sio wanachokitaka wao.
Muungano uliopo wa kijamii unatosha na wala hautovunjika; muungano wa kisiasa umalizike kwa kuipa nafasi kila nchi kuwa na uwakilishi kamili katika muungano uliopo wa Jumuia ya Afrika ya mashariki. Na wala hakuna haja ya kuonana maadui. Tuliungana kwa hiari(kama wanavyosema!), na pia tuachane kwa hiari kwa kuyaenzi mahusiano ya kale ya ujirani mwema.
Nawatakia kila la kheri Watanganyika katika uasisi wa taifa lenu jipya, na musinune mukaja kutunyima kutuuzia batata,tomato,karuti na kutukatia nyaya za umeme kama munavyotishia katika mitandao yenu (japokua huo umeme hamutupi burena hizo tomato na batata pia hamutupi bure). Nasi tutaendelea kuuenzi uhusiano uliopo wa maingiliano yetu ya karne na karne.
Idumu Zanzibar iliyo huru; Idumu Tanganyika iliyo jifukuwa huko iliko jifukia na kuwa huru.

No comments:

Post a Comment