Thursday, July 26, 2012

MANSOOR-SIMBA LIKINGURUMA MAFISI HUUFYATA MIKIA NA KUKIMBIA


Mweka Hazina wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid amesema yupo tayari kunyanganywa kadi ya chama hicho lakini hataregeza msimamo wake juu ya kuitetea Zanzibar katika Muungano. Kauli ya Mansoor imekuja siku chache baada ya chama hicho wilaya ya mjini kutoa maamuzi ya kuwataka viongozi wenye kupingana na msimamo wa chama kurejesha kadi za chama hicho au kuacha tabia hiyo mara moja.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Radio ya Ujerumani (DW) jana Mansoor alisema kamwe hawezi kuogopa vitisho vinavyotolewa na watu wenye kujipa madaraka na udikteta ambao hawataki mabadiliko wala mawazo tofauti.
Mansoor aliahidi kuendelea na msimamo wake katika kudai mabadiliko katika muundo wa Muungano na kusema kwamba msimamo wake hautabadilika licha ya vitisho vya baadhi ya Viongozi wa Chama hicho.
“Nimesema hayo tokea muda mrefu chama hiki kimetukuka na kina heshima na maadili yake ni baadhi ya watu wanataka kutuziba midomo lakini
Mimi sijasema leo nimesema tokea 2008-2009 juu ya msimamo wangu juu ya mfumo wa muungano na leo naendelea kusema tena hata ikipidi kunyanynganywa kadi mimi narejea tena kuwa mfumo huu wa serikali mbili sikubaliani nao na nitaendelea kusema ahivyo hivyo siwezi kubadilisha maoni yangu leo baada ya kuwa na msimamo miaka yote hayo” alisisitiza Himid ambaye ni Mjumbe wa NEC.
Aidha alisema Chama Cha Mapinduzi wilaya ya mjini hakina mamlaka ya kuitisha kikao na kutoa maamuzi kama hayo ambapo alisema ni watu wachache wenye nia ya kutaka kuwanyamazisha watu wenye maoni tofauti na wao.
“CCM wilaya ya mjini hawana mamlaka hayo, lakini pia hawana uwezo wa kutunyamazisha kwani CCM haijakataza wanachama wake kuwa na mawazo tofauti sasa nashangaa hao wanaosema sisi tumekiuka msimamo wa Chama ni msimamo upi maana mchakato wa katiba upo huru na kila mtu anatakiwa kutoa maoni yake” Alisema Himid.
Katika kuonesha kukasirika kwake na uamuzi huo wa kutaka kuwanyanganya kazi, Muweka Hazina huyo wa CCM alisema kwamba ni jambo la aibu kwa CCM Wilaya ya Mjini kufanya vitendo vya kibaguzi na vya udikteta kutaka kuwafunga midomo watu wasitoe maoni yao.
Alisema hakuna makosa kwa wana CCM kuwa na mawazo tofauti kwani kila mmoja ana haki ya kutoa maoni na kueleza msimamo wake na tabia ya kikundi cha watu kujiona wao ndio wenye mamlaka na wenye chama ni kosa na halipaswi kuachiwa.
Hao ni ni wabaguzi hawataki watu waseme ukisema unaonekana msaliti, hao ni watu wenye mawazo mgando hawataki kusikiliza fikra nyengine wanataka wanachosema wao ndio kiwe hicho hicho hilo haliwezekani na hatutakubali” Alisisitiza.
Hata hivyo alisema zama za kusema tunakwenda na fikra za mwenyekiti umepitwa na wakati na sasa jamii kubwa inakwenda na vijana amabo wanataka mabadiliko nchini hivyo aliwashauri wana CCM kuwaachia watu watoe maoni yao kwa uhuru kwani katiba tayari imetoa uhuru huo hivyo CCM hawawezi kuwa juu ya sheria.
“Hii nchi sio ya CCM peke yake hapa kuna CUF kuna Chadema na pia kuna vyama vyengine lakini wengine hawana hata vyama sasa hatuwezi kuendelea na watu ambao hawataki kuwa na mabadiliko wenye mawazo mgando …zama hizo zimeshapitwa na wakati wakati wa kwenda na fikra za mwenyekiti umekwisha” alisema Mansoor ambaye ni Waziri aisye na wizara maalumu.
Mmweka Hazina huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, alisema kitendo kilichofanywa cha kutishiwa kunyanganywa kadi ya CCM na baadhi ya viongozi hao ni cha fedheha na kimekitia aibu Chama cha CCM mbele ya wana jamii.
Himid alisema yeye ametokana na mifupa ya Chama cha Afro Shiraz (ASP) hivyo suala la kuwepo kwa dhana ya wanachama wa madaraja ndani ya CCM halipo kwa kuwa Chama hicho kinaheshimu misingi ya haki za binadamu na kuwataka wenye kudhani kwamba wao ndio wana mamalaka zaidi kuliko wengine waache tabia hiyo.
Hivi karibuni chama cha mapinduzi CCM wilaya ya mjini kilitoa tamko la kuwataka wajumbe wa baraza la wawakilishi, akiwemo Muweka Hazina wa CCM Zanzibar, Mansoour na makamo mwenyekiti wa CCM Zanzibar kuacha mara moja kukiuka maadili ya chama chao kwa kuwa na mtazamo hasi dhidi ya muungano.
Jana akihojiwa na DW, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisikika akisema kwamba viongozi wanaokwenda kinyume na madili ya chama chao watatakiwa kwenda kujieleza katika vikao na iwapo watathibitika wamekwenda kinyume basi watanyanganywa kazi au kufukuzwa.
Nape alisema mwana yoyote CCM hawezi kwenda kinyume na maadili ya chama chake na iwapo atakuwa na msimamo mwengine usiokuwa wa chama hicho basi atatakiwa kuwasilisha maoni yake ndani ya vikao na iwapo maoni hayo wajumbe hawatayaridhia basi atalazimika kurejesha kazi ya chama hicho iwapo yeye hatokubaliana na msimamo wa kikao.
Akijibu suala hilo Himid alisema kuwa Nape hawezi kugawa matabaka wanachama wa CCM, wale wa Tanzania Bara na Zanzibar kwani wote ni wanachama wanahaki sawa mbele ya sheria na katika CCM.
“Sisi Watanzania hatuna uhuru, yeye amegawa kwa utabaka, sisi ni watu wazima tuna haki na uhuru,  Nape hawezi kutwambia sisi watu wazima kwamba tukasema anayotaka yeye, ule wakati wa ndio Mwenyekiti haupo kila mtu ana haki yake kutoa maoni na hata Tume ya Jaji Warioba inasema hivyo” Alisema Himid. Na kuongeza kwamba.
“Mimi naichukulia kuwa hii ni njama ya kutaka kuwaziba midomo Wazanzibari, hatujakiuka miongozo wala sheria tutaendelea kusema kutaka mabadiliko ya muundo wa Muungano, hii nchi asilimia kubwa ni vijana na vijana wanataka mabadiliko na hilo haliwezi kukwepwa” Aliongeza.
Licha ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa mbali ya kueleza msimamo wa Chama hicho, lakini amesema wanachama wake hawafungiki kuwa na maoni na mitazamo tofauti katika mchakato wa katiba mpya.
“Mie nadhani kuna baadhi ya watu wana fikra za udikteta, haiwezekani twende kwenye kutoa maoni tukasema tunataka Serikali mbili kama ilivyosema CCM sisi ni watu wazima tuna haki zetu na tusichaguliwe la kusema na kwa nini tuzibwe au tufungwe midogo?” Alihoji.
Mansoor amesema msimamo wake kuhusu mfumo wa muundo wa Muungano utabakia kama ulivyo kutaka kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika muundo huo kwani kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka Zanzibar ambayo hayapatiwi ufumbuzi kutokana na kuwepo kwa muundo dhaifu wa Muungano.
Alisema hakuna mtu mwenye nia ya kuvunja Muungano, lakini ni lazima kukawepo kwa Muungano wenye maslahi ambayo hautakuwa na kero na ndio maana wamekuwa wakitoa maoni ya kutaka mabadiliko ya muundo na sio kuvunja.
“Mimi pia nakubali muungano una manufaa, lakini sikubaliani na mfumo wa Muungano na ndio maana tunasema kwa mfumo huu sebu(sitaki)” alisema Mweka Hazina wa CCM Zanzibar.
Tokea kuanza kwa machakato wa katiba wazanzibari wengin wamekuwa na maoni ya aina mbili tofauti ambapo wapo wengine wakitaka muungano kama ulivyo uendelee na wengine wakisema wanataka muungano wa serikali mbili zenye mamlaka kamili na zenye kuirejeshea Zanzibar ya kuingia mikataba na nchi za nje na baadae kuwe na mkataba.

No comments:

Post a Comment