Sunday, July 22, 2012

SIO TU HAMAD MASSOUD AJIUZULU LAA BALI SEREKALI NZIMA YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR WAJIUZULU


Ikiwa Waziri Mawasiliano na miundo mbinu atatakiwa ajiuzulu na mwenyewe binafsi akachukua uamuzi huo,itakuwa ni jambo la ajabu na hapana budi rekodi hio lazima iwekwe kwenye kitabu cha maajabu ya ulimwengu kwenye kumbukumbu ya Viongozi wa Afrika na utawala bora.Nasema hivi kwa sababu Waafrika hatuna utamaduni huo. Katika Nchi za Kiafrika na serikali zinazotawala kwa mabavu hili ni jambo la kawaida,mbona yanatokea mengi majanga ya aina hiyo. Hili sio suala geni,uzembe,rushwa na ubabe wa kutumia mabavu ndiyo mihimili ya serikali zetu.Nchi za aina hii fahari yake ni kupelekewa salam za rambi rambi na pesa za maafa kwa Viongozi wake baada ya tukio kutokea na sio kujikinga nalo.
Wazanzibar sifikirii kama wanapaswa kumshughulikia Hamad kama Hamadi,tukumbuke kwamba kidole kimoja hakivunji chawa. Tunapozungumzia suala hili, lazima lawama ziende kwa wote kuanzia sheha wa shehia mpaka kwa Rais Shein kwani yeye ndie mhusika na mhimili mkuu wa serikali. Sio vyema kumtupia Hamad massoud mpira pekee kama Hamadi wakati kosa hilo ni uzembe na utendaji mbaya wa Serikali mzima,kumlaumu Hamad pekee yake ni kutomtendea haki. Tatizo la kuzama kwa meli ni uzembe wa Serikali yote .Sifikirii kwamba hata boti za uokozi kukosa mafuta lazima waziri akasimamie hilo,sasa hivi huyu Waziri ana mikono mingapi na ajigawe vipande vingapi kama hata hilo lazima Waziri akalisimamie na kama hakwenda vyombo vitakosa mafuta,hivi ni vichekesho!
Tatizo letu sisi Wazanzibar nikuonesheana vidole kwa ubinafsi na chuki za kisiasa,lakini kile chanzo cha tatizo letu tunajaribu kulipuuza ,hatuna budi tuelewe kwamba Zanzibar hatuna Nchi wala utawala na wala kiongozi muadilifu, lakini hata hao Walioambiwa wamechaguliwa kwa magube basi haki haikutendeka katika uchaguzi na hili sote tunalijua,sasa kama ni hivyo unategemea vipi utendaji wao utakuwa,mpaka Nchi ipate maendeleo na tuepukane na majanga kama haya,ambayo ni tishio kwa Wazanzibar. Viongozi wa Zanzibar wanashughulikia mambo ya siasa zaidi ili wabaki madarakani lakini masuala yanayowagusa maendeleo na maslahi ya Wananchi hayo ni magumu kwao kufanyika.
Fikra zangu ni kwamba watu wengi wangekuja na hoja na mawazo ya kuishinikiza kujiuzulu kwa Rais wa Zanzibar na cabinet yake yote, matokeo yake wanamnyooshea kidole mtu mmoja tatizo jamani sio Hamad ,tatizo narudia tena kwamba ni Serikali mbovu inayoendeshwa na Dr Shein, ambayo inaongozwa na mtawala wetu Tanganyika.Si vyema kumtupia mtu mmoja lawama wakati tatizo letu tunalijua,ni uongozi mbovu.Katika serikali hii ambayo mambo yake yote yanaratibiwa kwa watawala wao,haya yanayo tokea ndio matunda yake,lililobaki tumshukuru Muumba lakini hili ni tatizo sugu kwa Wazanzibar na hatujui lini litamalizika, kwa sababu Wazanzibar wamegaiwa kivyama.
Mimi niulize suala moja Wazalendo,wale askari ambao wanawatesa na kuwanyanyasa Wazanzibar,waumini wa dini mpaka misikitini mwao,nao pia ni tatizo la Hamad na miundo mbinu yake? Jibu litakuja kwamba Serikali ndio mhusika wa yote yale. Tujaribuni kuwa wabunifu ili tuweze kuelewa chanzo cha matatizo yetu na sio kusema kwa jazba lakini ukweli tunauficha na kujitia pamba za masikio.Bado hatuna ndege zetu wenyewe lakini kama tungekuwa nazo basi hali ingelikuwa hivi hivi, ndege zingeanguka kila siku kwa mhusika kusahau kuweka mafuta ya kutosha tu,hivi ndivyo tulivyo.Umimi na uyakhe ndio unaotuongoza katika utendaji wetu. Sasa linapokuja suala la kwamba Waziri muhusika akakae chini ya tangi la mafuta kujua kwamba ndege imejaa mafuta au la, hilo haliwezekani lazima wahusika wawajibike,Waziri sio kila kitu akifanya yeye kuna watendaji na majukumu yao pia.
Dr. Shein amechaguliwa kwa mizengwe sio hivyo na hata hao Marais wengine waliopita ni hivyo hivyo,sasa katika hali kama hiyo tutegemee nini, isipokuwa uzembe kama huo ndio utendaji wa Serikali yetu tokea hapo awali.Hakuna mabadiliko ya watendaji yaliofanywa na Rais tokea kuchukua madaraka,isipokuwa alichokifanya ni kuzidisha watendaji wa zembe kwenye Mawizara na kuifanya Serikali yake kuwa kubwa kuliko Wananchi wake. Hata wale wakuu wa Mikoa na Wilaya Rais kashindwa kuwabadilisha sasa leo hii tunamlaumu mtu mmoja kwa kosa la Serikali mzima viereje,wote ni wahusika wanapaswa wajiuzulu kutokana na uzembe. Serikali kuonesha udhaifu wake ni kule kuendelea kukikodisha kisiwa cha chumbe kwa miaka mia,hivi hii ni Serikali au ni kampuni ya watu binafsi. Sehemu ile ni muhimu kuwekwa ”Police guard” kwa ajili ya uokozi,usalama wa nchi, matokeo yake mpaka msikiti pale umekabidhiwa wazungu wanakunywa pombe,wavuvi na raia wa Zanzibar wanashindwa kufika,watu wamefumba macho hilo halizungumzwi, hivi kweli tutafika ?.
Ukiwachilia hawa Mawaziri wachache wa C.U.F, Serikali na watendaji wake ni wale wale tuliowazoea wa chama tawala, kwa maana hiyo utendaji hapa haupo ndio maana nikasema kwamba Hamad Massoud hawashi wala hazimi ni kivuli tu katika Serikali hii Mapinduzi ya Zanzibar, ni sawa nakuchukua gunia la sukari na kulitupa nungwi ukafikiria kwamba maji yatageuka kuwa matamu hilo haliwezekani.Waswahili wanasema kamba hukatikia pabovu,ndio hili suala la kuzama kwa meli,lakini ukitaka ukweli ni kwamba Serikali yote haifai kuongoza imejaa madudu na haya Wazanzibar ndio tunayo yataka,wetu ni mdomo tu vitendo hamna. Matokeo kama haya yametokea mengi hapa visiwani,watu wengi wameuliwa hivi hivi na wala hakuna linalofanyika,uoga wetu ndio unaotuponza.Tunadanganywa kwa wimbo wa amani na utulivu huku tunamalizika mmoja baada ya mwengine. Hivi kama si uoga ni kitu gani ? Hawa askari wanaotesa ndugu zetu,mama zetu,dada zetu wanaishi mbinguni ?Kuna hatua yeyote tunayochukua kupinga dhulma hii,au ndio Mungu atatulipia ?
Kujiuzulu kwa Waziri sio suluhisho la Wazanzibar wala matatizo yetu,akiondoka leo kesho yake atakuja Hamad Massoud mwengine yatatokea yale yale kwani tatizo sio Waziri,tatizo ni Serikali kwamba haipo makini,Zanzibar ni mkoa wa Tanganyika kama vile Mtwara na kigoma.Tumeshindwa kijitawala leo tunatawaliwa lazima tukubali matokeo ya aina hii.Angalieni leo hii Zanzibar haina chake kila kitu unaambiwa hicho kinasimamiwa na Muungano lakini likitokea janga mpira unarushwa Zanzibar. Hivi ilipozama meli hii hawa watu wa hali ya hewa walikuwa wapi ? Jee kwa nini SUMTRA waliiruhusu meli kuondoka wakati wanajua kwamba bahari ni mbaya ? Baada ya kuzama kwa meli kwa nini waokozi wachukue masaa matatu kukifikia chombo ,Serikali na vikosi vyake vinafanya kazi gani? Kuna masuala mengi ya kujiuliza kabla kumuoneshea kidole mtu mmoja kisiasa.Ikiwa Zanzibar ni visiwa,serikali imejipanga vipi kukabiliana na hali za ajali kama hizi huku tukijuwa kwamba huu ndio usafiri wetu mkubwa ?
Serikali yetu ina udhaifu mkubwa kiasi ambacho hata ukihadithiwa kama wewe ni mgeni basi utashindwa kuelewa na hili ndio tatizo. Nchi yetu ni visiwa vidogo wananchi wake ni kidogo leo hii tunawatendaji kama vile Nchi kubwa zenye maendeleo makubwa,hili ni tatizo ndio maana kila moja anamtupia mpira mwenzake.Rais hakupaswa kuunda Serikali ya kizembe kama hii,hili ni tatizo kisaikolojia. Zanzibar kila kitu kinachofanyika lazima kiangaliwe kisiasa,nani kafanya, nani kasema,wapi anatokaka, jee rangi yake ni nyeupe buluu au nyeusi.Uongo,unafiki,fitna,majungu ndio unaotawala utendaji wa kila siku wa Serikali yetu ya Mapinduzi,anaepinduliwa siku zote ni Mzanzibar,wageni hapa ndio wanaokula nchi..
Ikiwa kweli Wazanzibar tunauchungu na Nchi yetu lazima tujitolee kwa hali na mali,maneno kwenye mtandao na hasira za mkizi hazitotusaidia kitu bado matatizo tunayo,matokeo yake yatakuwa ni faida ya Mvuvikupata kitoweo. Tuishinikize Serikali sio kwa maandamano tu bali kwa vitendo na mapambano ya mabavu kama yale wanayotumia askari wao. Wapemba na Waunguja tuungane kwa pamoja tupambane na adui yetu. Kwanza lazima taifa letu lipate heshima yake,lakini kubwa zaidi ni kutoa funzo kwa viongozi wetu ili mtawale mwengine yeyote atakae kuja ajue kwamba Wazanzibar wanataka heshima yao idumishwe na sio kuchezewa chezewa kizembe.

No comments:

Post a Comment