Wednesday, January 23, 2013

KARUME JR AOMBA KUPATIWA HATI HALISI YA MUUNGANO WA ZANZIBAR NA TANGANYIKA.JE IPO AU NDIO IMEFUKIWA GININGI..?



Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, ameomba kupatiwa hati halisi (Original) ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo imetiwa saini na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.
Ombi hilo la Karume limekuja kufuatia utoaji wake wa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, makamo Mwenyekiti Assa Rashid na wajumbe wengine aliyokutana nayo juzi nyumbani kwake Mjini Unguja.
Karume alisema yeye hana hati ya Muungano na hajawahi kuiona na iwapo Tume hiyo inayo hati hiyo basi angeomba kupatiwa kwani ni wazanzibari wengi wanahitaji kuiona hati hiyo ambayo ni mkataba kati ya nchi mbili zenye mamlaka kamili kila moja na zilizoungana mnamo mwaka 1964 kila nchi ikiwa huru.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya tume hiyo, kimesema Karume mbali ya kutaka kupatiwa hati ya Muungano lakini pia alisema anaunga mkono kuwepo kwa Muungano wa Mkataba ambao kila nchi itakuwa na mamlaka yake kamili na kisha kufuatia huo mkataba ambapo alisema Zanzibar kwa takriban miaka 50 sasa imekuwemo katika Muungano lakini imekuwa hainufaiki kiuchumi ndani ya Muungano huo.
Aidha Karume alisema yeye yupo tayari iwapo kutakuwepo na kipindi cha mpito kutoka Muungano huu uliopo na kuingia wa Makataba pale alipoulizwa na Mjumbe wa Tume hiyo, Salim Ahmed Salim ambaye alionesha khofu yake na uzoefu wa chaguzi zinazofanyika nchini kwamba zinakuwa na machafuko.
Karume alisema hakuna machafuko yoyote yatakayoweza kutokezea katika kipindi hicho cha mpito na iwapo Rais aliyekuwepo madarakani hataweza kusimamia na hatajiamini kwa hilo basi yeye anaweza kuchukua nafasi hiyo ili aweze kusimamia hilo na akaahidi kwamba hali itakuwa shuwari na kuivusha Zanzibar katika machafuko kama alivyoweza kusimamia Maridhiano kati ya vyama vikuu vya CCM na CUF mwanzo hadi mwisho wake.
Karume ambaye amekuwa rais kwa miaka 10 Zanzibar amesema amepata uzeofu mkubwa sana katika kipindi cha uongozi wake akiwa madarakani ambapo ameishuhudia Zanzibar ikidhoofika kiuchumi wakati upande wa pili wa Muungano ukinufaika zaidi.
Alisema ni wakati mwafaka kupitia katiba mpya watu kuwa wawazi na kusema ukweli kwa kubainisha kero na matatizo yote ya Muungano ili hatua za lazima zichukuliwe katika kuwaletea wananchi katiba iliyo nzuri na yenye usawa wa nchi mbili zilizoungana na zenye hadhi sawa.
Karume alisema waziwazi kwamba kwa kipindi cha miaka 10 ameshuhudia mengi sana katika suala zima la maslahi ya Zanzibar, lakini pia alisema sasa ni zama mpya za ukweli na uwazi na kwa hali iliyofikia sasa hakuna njia nyengine zaidi ya kila nchi – Zanzibar na Tanganyika – kurejesha mamlaka yake (sovereignty) kitaifa na kimataifa na kisha nchi hizo mbili kushirikiana kupitia Muungano wa Mkataba kati yao, hivyo ndivyo alivyosema Mheshimiwa Karume.
Hata hivyo Karume aliwaambia wajumbe wa tume hiyo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliotiwa saini na Mwalimu Nyerere na Mzee Karume ulikuwa na heshima hapo zamani na ukiheshimiwa sana lakini kumekuwepo na dharau fulani ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi na baadhi ya watendaji jambo ambalo linadhoofisha Muungano huo na kusababisha malalamiko makubwa miongoni mwa pande mbili hizo.

No comments:

Post a Comment