Monday, January 14, 2013

MAALIM SEIF AMPA UKWELI WARIOBA.AMWAMBIA KOTI LA MUUNGANO LINATUBANA.



MAKAMO wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema koti la Muungano kwa sasa linawabana Wazanzibari. Na kuongeza: Kwa kipindi cha miaka 49 ya Muungano huo bado hakuna nia njema.
Maalim Seif ambaye ni kiongozi wa kwanza wa juu wa Serikali kukutana na Tume hiyo katika utaratibu wa kukusanya maoni, alisema hakuna nia njema katika kutatua kero za Muungano, hali inayopelekea usumbufu kwa wananchi hasa upande wa Zanzibar.
Maalim Seif alikutana na Tume hiyo leo nyumbani kwake Mbweni, Unguja amapo alisema Muungano wa Serikali mbili uliyopo sasa hauwezi kutatua  kero zinazowakabili wananchi:
“Koti la Muungano linatubana sana na tunahitaji kushona koti jipya kulingana na hali zetu za sasa,” alisema Maalim Seif mbele ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba.
Alishauri kutokana na hali hiyo ni vyema muundo wa Muungano ukaangaliwa upya na kusisitiza msimamo wake wa kuwepo Muungano wa mkataba ambapo kila nchi itakuwa na mamlaka yake kamili:
“Tuna miaka 49 ya Muungano bila kuonyesha mafanikio ya kuridhisha ya kutatua kero za wananchi…sasa tunahitaji kushona koti, ili kila nchi iwe na mamlaka yake ya ndani na nje,” alisema Maalim Seif.
Alisema katika kipindi hicho Tume na Kamati kadhaa zimeundwa katika kushughulikia kero za Muungano, lakini mafanikio yake ni madogo, hali inayotia wasiwasi, kuongezeka kwa kero hizo badala ya kutatuliwa.
Maalim Seif alifahamisha, Zanzibar imekuwa muathirika mkubwa wa Muungano uliyopo, hasa katika nyanja za uchumi na siasa, baada mshirika wake ‘TANGANYIKA’ kutoweka, na kutumika jina la Tanzania kwa maslahi ya upande mmoja wa Muungano.
Maalim Seif ambaye pia ni katibu mkuu wa Chama cha wananchi (CUF) kesho anatarajiwa kukutana na waandishi wa habari katika hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar.
Aidha, Maalim Seif atatumia mkutano wake wa kesho, kuweza kufafanua maoni yake hayo na kuweka bayana kwa wananchi wote maelezo yake aliyoyatoa kwa Tume ya mabadiliko ya Katiba mpya.

No comments:

Post a Comment