Wednesday, February 20, 2013

WAKILI WA UAMSHO ATAKA KESI KUFUTWA MAANA UCHUNGUZI UNAOFANYWA KWA UPANDE WA MASHTAKA HAUKAMILIKI.



MAHAKAMA ya MATHALIM ya Wilaya ya Mwanakwerekwe imeombwa kuifuta kesi inayowakabili viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) kutokana na kuchukua muda mrefu kwa kesi hiyo bila ya ushahidi wake kukamilika na kila kukicha msemo ndio huwo huwo ushahidi haujakamilika.
Wakili wa washitakiwa hao, Salum Toufik alimuomba hakimu anaeiendesha kesi hiyo, Ame Msaraka Pinja kwamba kutokana na taratibu za kimahakama hususan katika makosa ya jinai kesi inapokuwa imefikia kuanzia miezi mitatu na kuendelea bila ya upelelezi kukamilika inapaswa kufutwa.
“Mheshimiwa mimi nahisi ni muda mrefu sasa wateja wangu wapo rumande na kesi kila siku upelelezi haujakamilika naiomba mahakama yako iangalie sheria na kanuni ili iweze kuifuta kesi hii,” alisema Towfik.
Kesi hiyo inayowakabili viongozi hao wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed ambao wanadaiwa kutenda kosa la uchochezi wa kufanya fujo kinyume na kifungu cha 45 (1)(a) na (b) sheria namba 6 ya mwaka 2004 walifikishwa tena jana katika mahakama hiyo kwa kutajwa.
Upande mashataka awali umeomba muda zaidi kuendelea na upelelezi wa kesi hiyo.
Upande huo ukiongozwa na Khamis Jafar wameiomba mahakama kuwapa muda zaidi baada ya upande wa watetezi wa washtakiwa kuiomba mahakama  hiyo kuifuta kesi hiyo kutokana na kuwa imekuwa kipindi kirefu pasipo na upelelezi kukamilika.
Hata hivyo, hakimu wa mahakama hiyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 19 mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa wamerejeshwa rumande hadi tarehe hiyo.
Washitakiwa hao ni Sheikh Farid Hadi, Mselem Ali, Mussa Juma, Azza Khalid Hamdan, Suleiman Juma, Khamis Ali na Hassan Bakari .
Mapema mwendesha mashtaka huyo alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao wakiwa ni wahadhiri kutoka Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya
Kiislamu walitoa matamko ya uchochezi yanayoashiria uvunjifu wa amani na kusasabisha fujo, maafa mbali mbali na mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na uharibifu wa mali za watu na serikali.
Wakati huo huo kesi nyingine inayowakabili viongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar juzi ilitajwa mbele ya hakimu mpya baada ya Hakimu Mohammed Ali Shein kujitoa katika kesi hiyo ya kufanya fujo.
Hakimu Shein alijitoa Desemba 27 mwaka jana katika kesi hiyo inayowakabili Sheikh Farid Hadi na wenzake sita iliyopo Mahakama ya Mwanakwerekwe mjini Zanzibar.
Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu wa Wilaya, Khamis Rashid ambapo washitakiwa wanne wako nje kwa dhamana na watatu bado wako mahabusu kutokana na kesi nyingine inayowakabli.
Washitakiwa watatu ambao walikwenda katika kesi hiyo wakitokea mahabusu ni Sheikh Farid, Juma Suleiman na Mussa Juma ambao wanakabiliwa na kesi Mahakama Kuu ya Vuga ambayo dhamana imefungwa.
Kesi hiyo ya Mwanakwerekwe inatarajiwa kutajwa Machi 4 na 5 na ile ya Mahakama Kuu itaendelea hapo kesho katika Mahakama ya Vuga Zanzibar.

No comments:

Post a Comment