Wednesday, March 20, 2013

MNAOLILIA URAISI NYAMAZENI MPISHENI DR SALIM AHMED SALIM AINGIE


Mnaolilia Urais Nyamazeni, Mpesheni Dk Salim Ahmed Salim Aingie

imeandikwa na Joseph Mihangwa.

PATASHIKA nguo chanika inaendelea kichini chini kwa vingunge wa vyama vya siasa kuendesha kampeni za urais kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015. Majina kadhaa yanatajwa na wao kutokanusha, na wapambe wao kuzizima.

Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanatajwa Waziri Mkuu Mstaafu (kwa kashfa), Edward Lowassa, Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na wengineo wachache.

Kwa vyama vya upinzani, anatajwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wakati kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), anatajwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba. Wote wanaojinasibu na kinyang’anyiro hicho, wanatoka Bara. Wazanzibari hawatajwi, kana kwamba Zanzibar si sehemu ya Tanzania.

Kwa CCM, ni utamaduni uliozoeleka kwa mgombea kutokana na Kamati Kuu ya Chama hicho, lakini kinyume na matarajio, hao wanaotajwa kuukamia urais wamefyekwa katika Kamati hiyo kwa sababu zisizofahamika.

Kuteuliwa kwenye Kamati Kuu ya CCM kwa mwanasiasa mkongwe na mwanadiplomasia wa kimataifa, Dk Salim Ahmed Salim bila matarajio ya makada wengi wa chama hicho, kumezua minong’ono, kiwewe na taharuki kwa wanyemeleaji wa nafasi hiyo kwamba huenda Dk Salim anaandaliwa kwa mambo makubwa zaidi.  Hata hivyo, wanajiliwaza kwamba kwa umri wake wa miaka 73, Dk Salim hizi si zama zake za kuongoza nchi!

Lakini pamoja na hayo, wanafahamu kwamba katika hali ya sasa ya taifa kupoteza dira na mwelekeo, panahitaji Rais makini kutawala awamu moja tu ili kuweka mambo sawa, bila kujali umri wala itikadi ya chama chake, mradi tu awe mzalendo na mkombozi wa wanyonge.

Lakini Mungu si Athumani; lolote laweza kutokea kwa mazingira ya sasa ya kuchafuka kwa bahari ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, hivyo kuhitaji nahodha mkongwe kuinusuru meli kwenye tufani. Tayari CCM imeweka wazi kuwa kinakusudia kurejea kwenye misingi ya uadilifu wa enzi za TANU na ASP ili kurejesha heshima ya taifa hili.

Ni nani awezaye kufufua misingi hiyo kwa uhakika na umakini mkubwa mbali na wa zama za Dk Salim Ahmed Salim? Jukumu hilo muhimu, kama tunavyoshuhudia, haliwezi kutekelezwa na wanasiasa wa zama za ‘Bongo fleva,’ au wale wanaotamba kwa ufisadi wao nchini. Taifa linayumba kwa kukosa viongozi wenye busara na hekima.


Taifa liko njia panda likiweweseka kwa dhambi kuu nne za maangamizi. Mosi; ni nchi kukosa itikadi na dira ya maendeleo. Tunaimbishwa Ujamaa huku tukichezeshwa ngoma ya Ubepari, ya kila mtu kuishi kwa ukali wa meno yake. Pili; ni kutoweka kwa maadili na utamaduni wa taifa hili kwamba nchi inabugia sumu, makapi ya kila aina kwa maangamizi yake. Nchi inapokosa utamaduni wake, ni sawa na mti usio na mizizi, kuweza kuangushwa na upepo duni tu.

Tatu; ni kutoweka kwa heshima ya Mtanzania katika duru za kimataifa, tofauti na enzi za Serikali ya awamu ya kwanza ambapo alisifika kama mpigania haki, usawa wa kijamii, amani na utulivu. Nne; ni kuibuka kwa udini unaotishia kuipasua nchi vipande vipande, na pengine kuitupa kwenye janga la umwagaji damu.

Tano; ni kero za Muungano ambapo Zanzibar sasa inataka itambuliwe kama nchi. Tayari Wazanzibari wamezika tofauti na uhasama wao wa siku nyingi na kufanikiwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa; uhasama uliowagawa na kuwadhoofisha kisiasa na kijamii kuweza kufinyangwa finyangwa ndani ya mfumo tata wa Muungano. 

Leo wanaweza kuzungumza kwa herufi kubwa ndani na nje ya Muungano; na tayari wamesema sasa ni zamu yao kutoa Rais wa Muungano. Je; Wabara ambao ndio walio wengi, watakubali hilo, katikati ya mikanganyiko ya kisiasa na kidini inayolikumba Taifa letu hili?

Misingi ya TANU na ASP ndiyo iliyozaa kile tunachojivunia sasa kama ‘hali ya amani na utulivu’ ambavyo vinatoweka haraka kutokana na uongozi wa nchi kuwa mikononi mwa nyang’au walafi na ubinafsi. Misingi hiyo ilikuwa ni usawa wa binadamu, vita dhidi ya rushwa, unyonyaji, uonevu na maisha bora kwa wote.

Chama Tawala kama CCM, hakiwezi kusalimika kama Chama iwapo wanachama wake, hasa viongozi, watautazama utendaji wake (Dk Salim) kwa maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya umma. Uanachama na uongozi wa aina hiyo, ni ugonjwa (ukoma) ndani ya Chama.


Kinachopotea haraka hivi sasa, kwanza; ni uhuru wa kitaifa, kwa maana ya uwezo wa wananchi kuamua juu ya hatima yao ya kujitawala bila kuingiliwa na watu wasio wazalendo. Pili; ni kupotea kwa uhuru dhidi ya njaa, magonjwa na umasikini kwa kuwa tu siasa, uchumi wa nchi na rasilimali za Taifa zimehodhiwa na kikundi kidogo cha wahujumu uchumi na mafisadi na Serikali ikasalimu amri kwa wadhalimu hao.

Tatu; ni kutoweka kwa uhuru binafsi, haki ya kuishi maisha ya heshima na usawa kwa wote, uhuru wa mawazo na wa kushiriki katika maamuzi yanayogusa maisha ya watu. Hivi leo,  mambo hayo ni kwa kudra ya Mungu, kwa kuwa kundi la walionacho halimjui mdunda kazi mwenye njaa. Na ingawa kuna Bunge linalopashwa kumsemea, limetekwa na ufisadi na kujipambanua kama taasisi ya ulaji na ya kuzika demokrasia.

Kurejea kwa wakongwe wenye kumbukumbu sahihi ya mambo haya kwenye ulingo wa CCM, kama vile Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mohamed Seif Khatib na wengineo, ambao hapo nyuma walipigwa buti kuachia nafasi vijana (ma-bongo fleva), ni ishara ya kutambua usemi kwamba ‘lazima utazame nyuma ili uweze kwenda mbele,’ na ni dalili pia ya kushindwa kwa kizazi kipya kuongoza nchi kwa mafanikio bila kuingiza busara na hekima ya wakongwe. 

Ilivyo sasa, CCM imegeuka kokoro lenye kuzoa kila uchafu na kutishia amani na usalama wa taifa kutokana na ukweli kwamba Chama lege lege huzaa Serikali legelege!

Kwanini tusiwe na kina Salim Ahmed Salim na kina Philip Mangula, Mohamed Seif Khatibu na wengineo wachache, kurejesha heshima ya Taifa hili baada ya kizazi cha ‘Bongo fleva’ kuonyesha wazi kushindwa kuhimili changamoto za utawala wa nchi?

Kuongoza nchi bila itikadi wala maadili ya taifa, ni sawa na nahodha asiyejua bandari aendayo. Kwa nahodha kama huyo, hakuna upepo ulio mwafaka kwake. Na ndimo tulimo hivi sasa, kwa nchi yetu kugeuzwa shamba la bibi pasipo mtu wa kukemea; uzalendo unayoyoma haraka kwamba tusishangae kuona siku moja Bunge likiongozwa na Spika Mjapani, au nchi kuwa na Waziri Mkuu Mmalaysia, kadri tunavyozidi kuruhusu nguvu ya fedha kuchukua nafasi ya uzalendo, kwani tayari wahaini hawa wanazungumzia uraia popo wa nchi mbili!

Nchi inakabiliwa na janga hatari jipya la mgawanyiko kwa misingi ya udini na uhasama unaokithiri, kati ya Wakristo na Waislamna kutishia amani. Haya yote ni ishara ya kudhoofika kwa uzalendo, umoja wa kitaifa na kiitikadi. 

Kama hali hii itaachwa kuendelea, uchaguzi mkuu ujao utakuwa mgumu kwa sababu kila kundi litataka achaguliwe Rais wa dini yake kwa gharama ya utaifa. Kwa hali ilivyo, hakuna mgombea mwingine anayeweza kuleta suluhu ya makundi haya mawili zaidi ya Dk Salim Ahmed Salim ambaye anakubalika kwa Wakristo na kwa Waislamu; tangu kale, juzi, jana hadi leo.

Dk Salim si mdini, si mhafidhina wa kisiasa, ni mwanademokrasia jamii. Kikundi cha Wazanzibari, kilichojiita ‘Liberators’ (Wakombozi) na kuzoea kumhujumu ili kulinda ‘ukale’ kinajua hilo na hakimuwezi tena.

Na kwa kuwa Wazanzibari sasa wamezika tofauti zao za kiitikadi za miongo mingi na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sasa ni dhahiri zile hujuma walizokuwa wakimfanyia Dk Salim, kwamba yeye ni mwanachama wa zamani wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) hazina mshiko tena. 

Kwa sababu hiyo, anaweza kuwa mgombea pekee wa urais, akipenda, anayekubalika vizuri na pande zote za Muungano pamoja na makundi ya kidini yanayoibuka kuliko mwanasiasa mwingine yeyote yule, Bara na Visiwani, licha ya umri wake mkubwa uraisi sio kubeba zegeeee.


Heshima ya Mtanzania imeporomoka mara dufu kimataifa tangu enzi za awamu ya pili. Kiongozi wa Kitanzania wa sasa si yule wa enzi za awamu ya kwanza, aliyechukia udhalimu, uonevu, unyanyasaji na ukoloni wa kimataifa, bali viongozi wa sasa ni mazuzu tegemezi, wasaliti na wakumbatia rushwa, ufisadi na mamluki wanaonunulika kirahisi kwa maangamizi ya nchi na wananchi.

Kuna mantiki gani kupinga maoni yaliyotolewa na Mwingereza, Bi Sarah Hermitage hivi karibuni kuhusu ufisadi, dhuluma na rushwa serikalini? Kuna mantiki gani kwa mafisadi wa nchi hii kuchochea vijana waandamane dhidi yake kwa madai ya kutudhalilisha badala ya kumsapoti?

Watuambie, iko wapi chenji ya vijisenti vya rada tuliyoambiwa vitalipwa..? Kwa nini tunaficha nyuso juu ya ufisadi mkubwa wa Meremeta, Richmond/Dowans, Deep Green na mwingine wa aina hiyo..? Wanafiki wapevu hawa! !!Wahaini, wasaliti wa taifa!!!! kama munataka raisi wa kweli ni Dk Salim Ahmed Salim tu lau kama munataka msaani wa BONGO FLEVA basi sawa chaguweni hao mafisadi waimalize kabisa nchi hii.

Tumejenga utamaduni tata wa kupata marais kutokana na mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje, kuanzia na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Rais wa sasa Jakaya Kikwete; na leo Waziri wa sasa wa wizara hiyo, Bernard Membe anapiga jaramba kufuata nyayo. 

Yote haya eti ni kwa lengo la kutia ubani uvundo wa nchi katika medani za kimataifa! Kama kweli hiyo sasa ndiyo tiketi ya urais, basi hakuna Mtanzania aliye hai wa kuweza kumfikia Mwanadiplomasia Dk Salim Ahmed Salim!

Dk Salim Ahmed Salim, kama alivyokuwa Mwalimu Julius Nyerere, ni mwanasiasa, mwanadiplomasia wa kimataifa na msomi mwenye historia ndefu ya harakati za mapambano dhidi ya uonevu; mwenye kiu ya haki na usawa kwa wote. Wengi tunamkumbuka miaka ya karibuni kama Balozi, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (sasa Umoja wa Afrika) na msuluhishi wa migogoro kimataifa.

Mwamko wake wa kisiasa unaanzia miaka ya 1950 huko Zanzibar enzi za mapambano ya kudai uhuru wa visiwa hivyo, kama Katibu Mwenezi wa Umoja wa Vijana uliojulikana kama Youths Own Union (YOU), uliounga mkono harakati za chama cha mrengo wa kushoto cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP).

Wakati huo, vijana wa Kizanzibari walijipambanua na harakati za kupinga ukoloni kitaifa na kimataifa, kuanzia harakati nchini Algeria dhidi ya ukoloni wa Kifaransa, na Ghana dhidi ya Waingereza, Mau Mau (Kenya) na Afrika kusini dhidi ya tawala za kibaguzi za Wazungu, na kutoka harakati za ukombozi wa Wapalestina hadi vita ya Vietnam, kwanza dhidi ya Wafaransa na baadaye Marekani.


Dk Salim, kama msemaji wa YOU, alikuwa mtu wa kwanza Afrika Mashariki kutahadharisha juu ya uwezekano wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Congo, Patrice Emery Lumumba, kuuawa na mabeberu, ilipotangazwa kwamba amepotea. Alishambulia (Dk Salim) vikali Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa hujuma hiyo; na leo historia imethibitisha kuwa alikuwa sahihi.

Ni Dk Salim aliyewaongoza vijana wa Kizanzibari kupinga hatua ya Marekani kujenga Kituo cha Kijasusi (tracking station) Zanzibar sehemu ya Tunguu, hadi kikaondolewa. Ni katika harakati hizi dhidi ya ukoloni na ubeberu, alikutana na mwandani wake, Mama Amne Ali Rifai wakaoana.

Ni kutokana na kuundwa kwa chama cha harakati za ukombozi cha Umma Party visiwani Zanzibar, kwa vijana wanaharakati kujiengua kutoka ZNP, wakiongozwa na Abdulrahman Babu mwaka 1963, kwamba Dk Salim alianza mikiki mikiki ya kibalozi, kwanza nchini Cuba na baadaye Misri. 

Alikuwa Cuba wakati Rais wa nchi hiyo, Fidel Castro alipotangaza azimio lake mashuhuri la Havana (the Havana Declaration), na Dk Salim akalikariri sehemu zake muhimu kwa lugha ya Kihispaniola. Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, Serikali mpya ya Mapinduzi ilimteua kuwa Balozi nchini Misri akiwa na umri wa miaka 22 tu. Na Muungano waTanganyika na Zanzibar ulipozaliwa, Aprili 1964 alibakia Misri kama Balozi wa Tanzania.

Alitumika kama Balozi kwa mara ya mwisho nchini China ambako alikuwa rafiki kipenzi cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Chou-en-Lai, kabla ya kuteuliwa Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), alikotumikia kwa miaka kumi. 

Akiwa huko, alitoa mchango mkubwa na kuiletea heshima kubwa nchi yetu, kwanza kwa kuchaguliwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya UN ya Ukombozi dhidi ya Ukoloni, kisha Rais wa Baraza la Usalama la UN na Rais pia wa Baraza Kuu la Umoja huo. 

Aliwania nafasi ya Katibu Mkuu waUN na kuungwa mkono na mataifa yote wanachama, lakini alishindwa kwa kura turufu (Veto) ya Marekani kwa sababu tu alijipambanua na siasa za mrengo wa Kisoshalisti. Ndiyo kusema kwamba mchango wa Dk Salim kwa ukombozi wa Bara la Afrika na dunia kwa ujumla, hauwezi kupuuzwa wala kusahaulika.

Kama Watanzania wanatafuta Rais wa kurejesha amani na utulivu, mshikamano wa kitaifa, usawa na demokrasia ya kweli nchini na heshima inayopotea, ni nani zaidi ya Mtanzania huyu asiyejua lugha ya ulafi, ufisadi, udini wala kulipiza kisasi, Dk Salim Ahmed Salim? Tunahitaji mtu wa aina yake kwa kipindi kimoja tu cha uongozi kunusuru nchi yetu!

Mwisho.

No comments:

Post a Comment