Tuesday, April 30, 2013

MIAKA 49 YAMUUNGANO: MASWALI SITA NA MAJIBU YA KIPUMBAVU


Makala hii nimeinakili kutoka blog ya Zanzibar ni kwetu. Toa maoni yako
¤Kwenye kuingia mkataba wa Muungano, kwa nini Nyerere alimshirikisha mwanasheria wake Roland Brown wakati Karume alimpa mwanasheria wake Wolfgang Dourado likizo ya muda kwenda nchini Uganda wakati Karume hakuwa msomi ukiachia uzoefu wa kazi ya ubaharia pamoja na umaarufu wa kucheza mpira?
Nyerere alimshirikisha mwanasheria wake huyu kwa sababu andiye aliyekuwa mwanasheria wake. Tanganyika haikuwa na wanasheria wa kabila ile wakati ule. Karume alikuwa Rais aliyemteua Dourado kuwa mwanasheria mkuu na alikuwa na mamlaka ya kumtoa cheo hicho au kumpeleka likizo. Aidha, kwa kuwa mwanasheria ni mtumishi wa mteja wake, hana maamuzi yoyote nje ya yale anayotaka mteja wake; hivyo kama Dourado hakukidhi mahitaji/matakwa ya Karume, alipaswa kuwekwa kando kwa mtindo wowote ule. Wanasheria ni matarishi tu wa wateja wao katika ufundi wa sharia.
¤Hati ya Muungano ilikuwa na mambo 11. Hivi sasa yamefikia 23 kutokana na kuongezwa na Nyerere taratibu kwa kupitia decree. Je, Karume alijua kuhusu uwepo wa decree kwenye katiba?
Ni kweli mambo ya Muungano yamefikia 23 kutoka 11 ya awali. Kuna sababu zake, mojawapo ikiwa kwamba hakukuwa na makubaliano ya kubakia na yale yale 11 bali kulikuwa na makubaliano ya kuuboresha Muungano. Pili, si kweli kwamba ni Nyerere pekee aliyeyaongeza, au tuseme kwamba yaliongezeka wakati wa Nyerere tu. Soma historia ya Muungano ujielimishe. Aidha, Karume alikuwa shuhuda wa kuongezwa mambo ya awali, mfano baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa sarafu ya Afrika Mashariki na kisha kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania. Mambo haya yameongezeka kutokana na ulazima wake, umuhimu wake, na yalifuatwa utaratibu kila yalipoongezwa. Kumbuka, mambo ya Muungano yanasimamiwa na serikali ya Muungano, Rais wa Muungano na Bunge la Muungano, si nje ya hapo. Ili kufahamu sababu za kila jambo liliongezwa, anzia na tovuti ya Makamu wa Rais, kisha ukikwama, uliza.
¤Mkataba wa Muungano uliridhiwa na Bunge la Tanganyika (tena weekend). Kwa nini Bunge la Zanzibar (Baraza la Mapinduzi) halikuwahi kukutana kuridhia? Je, Muungano ni halali?
Bunge lilikuwa na uwezo wa kukaa siku yoyote. Lingekaa Jumatatu ingebadili nini? Zanzibar haikuwa na Bunge halali. Hata hivyo, Baraza la Mapinduzi lilipitisha muswada wa Muungano ila kusichokuwepo ni rekodi. Muungano ni halali na nakala yake iko Umoja wa Mataifa, New York ambapo hawapokei mikataba magumashi.
¤Karume hakutaka muungano wa serikali mbili. Ilikuwaje Nyerere akakomaa?
Ukweli ni kwamba Karume alitaka serikali MOJA tu akisema, “Nyerere wewe kuwa rais, mimi Makamo”. Walizungumza na wakakubaliana kuunda serikali mbili na Karume akawa Makamu na miaka yote ya uhai wake hakupinga uwepo wa serikali mbili. Kudai hivyo ulivyosema ni mzaha.
¤Kama lengo la Muungano ni regional integration (as opposed to Kwame Nkurumah’s notion), kwa nini Muungano wetu haukuongezeka tena tokea 1964 (e.g. Kwa ku-include nchi za jirani e.g. Mozambique au Zambia? Je, ni kwa sababu waliona matatizo makubwa kwenye muungano wetu (kama Ethiopia/Eritrea, Sudan/South Sudan, Gambia/Senegal).
Lengo la Muungano halikuwa regional integration na wala haukufanyika ili kupingana na wazo la kidikteta la Nkrumah. Ili Muungano wa kikanda utokee ilipaswa kutimia ile ndoto ya Afrika Mashariki. Baada ya hoja hii swali linafia hapo hapo. Nenda kawaulize hao wengine sababu zao.
¤Kwa mazingira ya hivi sasa ambayo uwezekano wa kupata rais mzanzibar kuzidi kuwa mdogo, je, muungano unaweza kudumu miaka mingi mingine?
Rais wa Muungano kutoka Zanzibar ni jambo linalowezekana; si kweli kwamba haiwezekani. Mfano, kama Dkt. Salim Ahmed Salim asingepingwa na Wazanzibari kila anapojaribu, angekuwa Rais wa tatu (kama asingegoma kuweka jina lake) ama wa nne wa Muungano (kama angepata kura za kutosha). Aidha, muungano haupaswi kulindwa na zamu za urais. Urais ni taasisi nyeti, hatuwezi kupekezana kama njugu. Hii siyo kwenye Muungano tu, bali hata kwenye masuala mengine kama udini, ukabila, jinsia, umri, n.k.

No comments:

Post a Comment