Monday, August 19, 2013

MAJUWA WALIVYO KUTANA KISIWANDUI KUPANGA KUMTIMUWA MANSOUR YUSUPH HIMIDI


Kamati maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM MAJUHA nchini Zanzibar, imepitisha pendekezo la kumvua uanachama Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamiki na Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mansoor Yusuph Himid tishio kwa wahafidhina, huku wajumbe wengine wakimshutumu Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi ya Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad atii kwa kauli zake zinazoteteresha umoja wa kitaifa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho cha MAJUHA kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Ali Mohamed Shein na kumalizika usiku mkubwa juzi katika ofisi za makao makuu ya CCM zilizopo Kisiwandui, zinaeleza kuwa wajumbe wa NEC wakiwemo Wabunge, Wawakilishi walisema Mansoor atii ameshindwa kulinda sera na ilani ya uchaguzi ya chama hicho kutokana na msimamo wake wa kutetea mamlaka kamili ya NCHI YA Zanzibar.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini  Borafia Silima Juma alisimama na kutoa pendekezo la kutaka kufukuzwa uanachama Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki(CCM) Mansoor Yusuf Himid kwa madai amekwenda kinyume na sera ya chama hicho kwa kushirikiana na wapinzani.
Borafia alisema tokea awali Mansoor hakuwa mwanachama wa CCM bali aliingizwa na shemeji yake ambaye alikuwa Rais wa nchi ya ZaNzibar awamu ya sita Dk Amani Karume, kumpa madarakana huku akifahamika ni mfuasi wa chama pinzani.
Makamo Mwenyekiti wa Wazazi Zanzibar Dogo Idd Mabruk alisema umaarufu wa Mansoor kisiasa ulitokana na nguvu ya CCM lakini hana ubavu wa kushinda uwakilishi jimbo la Kiembesamaki hata akifukuzwa uanachama leo.
Dogo alisema kuwa hakuna haja ya kuendelea kumbembeleza mwanachama ambaye si mtii wa katiba ya CCM na misimamo yake na kueleza kuwa kubaki na aina ya wanachama hao ni hatari kwa uhai wa CCM.
Hata hivyo Mjumbe Machano Othman Said ambaye ni Waziri asie na Wizara Maalum na Mwakilishi wa jimbo la Chumbuni amekieleza kikao hicho kuwa kupitisha uamuzi wa kumvua uanachama Mansoor peke yake kwa madai ya kuzungumzia sera ya Muungano wa Serikali tatu hautakuwa na maana yeyote bila ya kuitwa na wanachama wengine ambao wamelizungumzia suala hilo.
Machano alisema “ikiwa kweli wajumbe wanamtupia lawama Mwakilshi huyo na kutaka afukuzwe uanachama ni vyema na wengine waliotaoa maoni kama hayo wakaitwa ili washitakiwe badala ya kumuadhibu peke yake” alisema Machano ambaye alipikika kisiasa wakati wa utawala wa Dk.Amani Abeid Karume. “Waliotoa maoni ya kutaka Serikali tatu ni wengi, wengine ni Wawakilishi Na Mawaziri ,wanafahamika kwa majina yao , wote waitwe na si kumtoa kafara peke yake, huo utakuwa ni uonevu”Alisema Machano.
Mwakilishi huyo wa jimbo la Kiembesamaki Masoor Yusuph Himid ni mtoto wa muasisi wa Mapinduzi ya nchi ya Zanzibar ambaye pia ni shemeji yake Rais wa awamu ya sita Dk.AMani Abeid Karume, ni miongoni mwa wanasiasa wanaotetea mamlaka kamili ya nchi ya Zanzibar chini ya kamati ya maridhiano yenye wajumbe sita watatu kutoka CCM na wengine CUF.
Mansoor Yusuph Himid ni kiongozi wa kwanza kuchukuliwa hatua ya kutaka kufukuzwa, kutokana na misimamo yake ya kupinga mfumo wa serikali mbili, pamoja na chimbuko la suala la mafuta na gesi asilia kutaka kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano na kufika mbali zaidi kwa kueleza kuwa Muungano huo ni sawa na ukoloni mambo leo na wizi wa mchana kwa kutaka rasilimali za Zanzibar kunufaisha Tanganyika  (Tanzania).
Alipoulizwa kuhusu yaliyoamuliwa katika kamati kuu dhidi yake, Mansoor alisema kauli hizo yeye pia amezisikia kwa watu na hajataarifa rasmi hivyo hawezi kutoa maoni yoyote. “Mie nashukuru Mwenyezi Mungu bado mzima na wewe mzima kwa hili bado mapema kulitolea msimamo wangu, kwa sababu nimelisikia kama ulivyolisikia wewe, hivyo ‘No Coment” alisema Masnour ambaye alivuliwa Uwaziri na Shein.
Wakati hayo yakitokea Serikali ya umoja wa kitaifa ikapewa angalizo na baadhi ya wajumbe wa NEC kuwa makini na mwenendo wa utendaji kazi wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi ya Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad kuwa hausaidii kujenga umoja wa kitaifa na kufikia lengo la kumaliza matatizo ya kisiasa nchini  Zanzibar.
Mkuu wa Wilaya wa zamani na Mjumbe wa NEC Usi Yahya alisimama na kumueleza Shein kuwa ukimya wake dhidi ya wapinzani na hali ya siasa ilivyo nchini  Zanzibar kuna tishio na jaribio la kukichimbia kaburi chama tawala kishindwe katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Yahya alinukuliwa akisema kwamba matamshi ya Makamo wa Kwanza wa Rais nchi Zanzibar Seif Shariff Hamad dhidi ya Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Shein , si yenye nia njema na kitendo cha Shein kukaa kimya bila ya kumchukuilia hatua za kinidhamu ni aibu machoni mwa wafuasi wa CCM.
“Nakuomba  Shein umeichukua nchi ikiwa salama, ukimya wako na woga utakizamisha chama chetu, hebu amka na changamka, humjui Seif, kamuulize Mzee Jumbe, huyu ni hatari na hatabiriki na hutamfahamu ”Alisikika akisema Yahya.
Alifika mbali zaidi kwa kueleza kuwa kilichounganishwa ni kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini zanzibar na si kuunganishwa kwa sera za vyama vya CCM na CUF hivyo anachokifanya Maalim Seif na mawaziri wake ni mkakati wa kumbomoa Shein na kukimegua Chama Cha Mapinduzi.
Aidha mjumbe mwingine ambaye ni mbunge wa jimbo la Magomeni Amour Chombo alisimama na kumpasulia Shein kuwa mchezo wa kukigeuza kisiwa cha Unguja ni uwanja wa mapambano na Pemba ikibaki salama ni ajenda ya siri inayowakera wananchi wa Unguja.
Chombo alisema kimsingi hakuna mkataba wa Muungano kati ya visiwa vya Unguja na Pemba na uamuzi wa baadhi ya wanasiasa hasa wa CUF ambao wengi ni wapemba kuhoji hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni chokochoko za kisiasa na si jambo jingine.
“Hapa tulipofika hebu natuseme basi yatosha , imekinaisha ,tumevumilia vya kutosha,hakuna haja hadi watu waje kumwaga damu na kuuana kama Burundi , Pemba na Unguja ziwe mbalimbali, tindikali, fujo na ghasia kwanini zitokee Unguja kila siku ”Alinukuliwa Chombo akisema
Chombo alisema kwanza hakuna hati ya Muungano rasmi kama ule wa Tanganyika na Unguja ya mwaka 1964 , Pemba iwe Pemba na Unguja ni vyema ikabaki kivyake kwa kuwa hakuna nia njema na tija ya kisiasa.
Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM inadaiwa alilazimika kukabili hoja zilizojitokeza na kuzijibu kwa ufasaha ikiwemo suala la kuhoji muungano wa visiwa vya Unguja na Pemba ambapo alidai kuwa CCM haiwezi kukosa fadhila kwa vile ilifanikiwa kuchota kura 23,000 zilizomsaidia mgombea wake Shein kupata ushindi katika uchaguzi huo kutoka kisiwani Pemba.
Vuai aliwataka wajumbe wa kikao hicho kutoa hoja zitakazosaidia kusukuma kasi ya maendeleo badala ya kuyapa nafasi mambo yanayoweza kuzorotesha umoja wa kitaifa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment