Sunday, August 18, 2013

MWANA SHERIA MKUU WA NCHI YA ZANZIBAR ASEMA WENGI WANAOTAKA SERIKALI MBILI WANALINDA MASLAHI YAO YA KIDUNIA

Mwanasheria Mkuu Zanzibar Mh. Hamad Masoud .Mwanasheria Mkuu wa nchi ya Zanzibar Mh. Hamad Masoud
 Awashangaa wanaotaka Zanzibar iendelee kuwa manispaa
Asema kutokuwepo Serikali ya Tanganyika ndio kero Kuu ya Muungano
 Awasuta wanaotaka Serikali Mbili
Mwanaseria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar leo amesema lengo la kuandikwa kwa Katiba Mpya si kuyafanyia Marekebisho katiba iliyokuwepo sasa bali ni kandika Katiba Mpya katiba ambayo itakuwa muarubaini kwa kero za Muungano na Muungano wenyewe.
Mwanasheria Mkuu wa nchi ya Zanzibar aliyasema hayo leo asubuhi alipokuwa akifunguwa Baraza la Katiba la Vyuo Vikuu liliondaliwa na ZAHILFE Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Zanzibar liliofanyika katika Ukumbi wa Salama Bwawani.
Alilisifu Baraza hilo na kusema kuwa ni Baraza la Vijana wasomi na kuwasifu Vijana kwa ile sifa yao kubwa ya kuleta mapinduzi katika jamii yoyote.
Alimtaja kijana Sir King ndiye aliyesababisha Zanzibar iiteme Tanganyika mwaka 1895 Ogasti na Tanganyika kuangukia katika mikono ya Wajerumani.
Na kumtaja Gerald Pota aliyetumwa na Waingereza kuja kuunda Serikali na kumpangia Mfalme mshahara ambako alikuwa akilipwa paund 250 kwa mwaka.
Msingi wa Muungano wa (Tanzania) ni kuungana kwa Nchi mbili huru Tanganyika na Zanzibar lengo la kuungana kwa nchi mbili hizi ni kufanya mambo yao pamoja na kupata faida zaidi na sio Nchi moja kuitawala Nchi nyengine alisema, hukua akiendela kusema Mwana Sheria huyo Mkuu wa nchi ya Zanzibar:
Zanzibar si mkoa wala wilaya, Zanzibar ni Nchi, katika Muungano tulikubaliana baadhi ya mambo kufanya pamoja na sio Zanzibar kuwa jimbo la Tanganyika.
Alisema duniani kuna miungano mingi mizuri akiutolea mfano Muungano wa Uswisi ambao una Serikali 24 na ule wa Muungano wa Marekani wenye Serikali 52 na kusema kuwa ni uongo kuwa Serikali Tatu zitavunja Muungano na kusema Serikali Mbili ndizo zitakazovunja Muungano, na hata Muungano wa Serikali Tatu ukivunjika si kioja.
Serikali Tatu hazitovunja Muungano Serikali Mbili ndizo zitakazo vunja Muungano.
Alisema Uruhani wa Serikali ya Tanganyika ndio kero kubwa ya Muungano na Serikali tatu itairudisha Serikali ya Tanganyika ambako kero kubwa itakuwa ishatatuliwa.
Aliitaja Sheria ya Kuanzishwa na Benki Kuu ya (Tanzania) kuwa aliisaini Karume mwenyewe lakini Karume alipoona mapungufu ya Sheria hiyo ndio maana akaanzisha Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).
Aidha alisema kama Zanzibar inataka kuishtaki TFF itashinda na TFF haitokuwemo FIFA kwani TFF haiwakilishi (Tanzania) kama ilivyokuwa ZFA ilivyokuwa haiwakilishi (Tanzania).
“Hivi hatuoni haya kubakia hivi hivi kuwa Manispaa wakati Zanzibar ilikuwa Empire...??? Alihoji Mwanasheria Mkuu wa nchi ya Zanzibar na kuendelea kusema “hivi tutamuamini vipi mtu ambae leo anasema Zanzibar si Nchi atakapokuwa Rais wa (Tanzania) ambao Zanzibar haitokuwa na Mamlaka atasema Zanzibar ni jimbo la Tanganyika…” na kumalizia kusema wengi wa Watanganyika wanachuki na Zanzibar.
Aliwataka wanafunzi hao kuzungumzia mambo ya Muungano na kutaka kuwe na usawa “Bila ya kuwa na usawa katika Mungano huu, huo si Muungano bali ni ukoloni” alisema Mwana Sheria Mkuu wa nchi ya Zanzibar, na kutaka kuwe na mfumo wa usawa katika Baraza la Mawaziri na Bunge na kuwe na makubaliano ya thuluthi mbili kila upande katika kupitisha sheria na kuengezwa au kupunguzwa mambo ya Muungano.
Alisema katika Muungano wa Serikali Tatu ni lazima Rasilimali zitumike kwa Usawa na sio kama hivi sasa Tanganyika inavyotumia Rasilimali za Muungano wao peke yao katika kusoma na kuinyima Zanzibar.
Tume ya Pamoja ya Fedha haijaanza kazi mpaka leo, na katika Muungano kuna mapato ya Muungano na Matumizi ya Muungano na Mapato ya Muungano siku zote huwa mengi ambako Tanganyika hawataki tugawane.
Alisema si kweli kama Muungano wa Serikali tatu una gharama bali Muungano wa Serikali Mbili ndio wenye gharama na Zanzibar ndio inagharamika zaidi, aliwataka viongozi wawe wakweli na waache kuwapotosha wananchi.
Aliwaonya Wazanzibari kuacha kulumbana na badala yake kukaa pamoja kuidai nchi yao.
Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa ili kuondoa tofauti kwa Wazanibari na kusema kuwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni suala gumu kuliko mabadiliko ya Muungano.
Alisema Wanaotaka Seriakali Mbili hoja zao hazina msingi na hakuna haja ya kubakia kwenye Serikali mbili na wengi wanaotaka Serikali Mbili wanalinda maslahi yao ya kidunia.
“Hoja yangu nawataka wanaotaka Serikali Mbili na Wanaotaka Mkataba wakae pamoja wajadiliane Mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu mfumo ambao utakuwa na maslahi na Zanzibar.
Awali Mwenyekiti wa ZAHILFE alikanusha taasisi yake kuandaa kungamano la tarehe 6 mwezi wa 7 lililofanyika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni na badala yake kongamano hilo liliandaliwa na Mkoa wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya CCM na kusema Taasisi yake haina mafungamano na chama chochote cha siasa.
Kongamano hilo lilianza na Wimbo wa Taifa wa Zanzibar na lilihudhuriwa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Marais 10 wa Serikali za Wanafunzi waliochangia katika Kongamano hilo walitaka Zanzibar yenye Mamlaka Kamili na Usawa Katika Muungano.

No comments:

Post a Comment