Wednesday, August 14, 2013

SHEIKH MPONDA AONGEA KIDOGO



Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini 

Tanganyika, Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa na mkewe 

Hadija Ahamad 


alipomtembelea jana.

Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Tanganyika, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema alichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kujielewa kwa muda baada ya kupigwa risasi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu katika wodi binafsi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) alikolazwa jana, Sheikh Ponda alisema kutokana na hali hiyo hakumbuki matukio yaliyofuata baada ya hapo.
“Sikumbuki hata nilipata huduma ya kwanza hospitali gani kwa sababu sikuwa katika hali ya kawaida. Mambo mengine yaliyotendeka kabla ya kujeruhiwa ninayakumbuka vizuri,” alisema Sheikh Ponda ambaye inasadikiwa kwamba alipigwa risasi na polisi ya begani, Ijumaa iliyopita mjini Morogoro.
Alisema alihutubia katika Kongamano la Waislamu kwa muda mfupi akizingatia muda uliokuwa umetolewa kumaliza mkutano huo na baada ya hapo alishuka na kupanda kwenye gari binafsi ambalo lilizingirwa na polisi ndipo akaamua kushuka na kuanza kutembea kabla ya kujeruhiwa.
Mahojiano maalumu na Sheikh Ponda
Swali: Je, watu waliokupa huduma ya kwanza mara baada ya kujeruhiwa walikuta risasi iliyokujeruhi..??
Jibu: Nilipigwa risasi kwa nyuma ikatokea mbele kwa hiyo haikubaki mwilini wala haikuonekana ilipoangukia kwa wakati huo maana kulikuwa na purukushani.
Swali: Ulipata wapi huduma ya kwanza..??
Jibu: Kwa kweli kwa sasa siwezi kukumbuka nilihudumiwa wapi kwa sababu mara baada ya kujeruhiwa sikuwa katika hali yangu ya kawaida, nilichanganyikiwa.
Swali: Utathibitisha vipi kama ulipigwa risasi...??
Jibu: Bahati nzuri ni kwamba tukio hili lilitokea kweupe wapo wengi walioshuhudia, kwa hiyo wanaweza kusaidia kuthibitisha na ushahidi mwingine ni jeraha hili.
Swali: Nini msimamo wako baada ya tukio..??
 Jibu: Nitaendelea kuzungumzia haki za Waislamu na siwezi kurudi nyuma. Pamoja na kwamba wananiona mimi ni mtu mchochezi lakini wanaeneza chuki dhidi yangu kwa njia wanazojua wao. Nitaendelea, risasi haitaninyamazisha.
Swali: Umehusishwa kufanya uchochezi Zanzibar, unalizungumzia vipi hilo..??
Jibu: Zanzibar nilichozungumza ni kuhusu kesi dhidi ya viongozi wa Kundi la Uamsho. Watu wamewekwa ndani kwa miezi tisa sasa, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, kesi wanayoshtakiwa ina dhamana, sasa nikauliza kwa hao viongozi, kwa nini hawazingatii sheria..?? Kesi zina muda mrefu hazitolewi uamuzi, nikawasisitiza wazingatie misingi ya sheria kwa kuwa hivyo wanavyowatendea wananchi wajue kwamba hawastahili kupewa tena ridhaa ya kuongoza nchi, nilifikisha ujumbe wangu.
Swali: Kuna tukio la kumwagiwa tindikali mabinti wawili wa Uingereza lililotokea Zanzibar, ambalo wewe pia unahusishwa, hili unalizungumziaje..??
Jibu: Sijaona huo ushahidi ambao wanahangaika kunihusisha na tukio hilo, nahusishwa vipi..?? Matukio ya kumwagiwa tindikali yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara huko kabla sijakwenda kuhutubia. Vyombo vya dola vifanye kazi yake vyema ili kubaini ukweli wa jambo hili.
 Mke wake, Sheikh Ponda, Hadija Ahmad ambaye alikuwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa mumewe nae akaulizwa.
Swali: Unazungumziaje tukio hili la kujeruhiwa kwa mumeo..??
Jibu: Hili ni dhumuni la Serikali, lililenga moja kwa moja kumdhuru ili kunyamazisha harakati zake za kutetea wanyonge. Ni tukio la kupangwa, halijatokea bahati mbaya. Serikali inamfuatilia sana hivyo ililenga kumnyamazisha.
Jibu likiendelea; Namshauri Rais (Jakaya Kikwete), kuhakikisha kwamba haki za wanyonge zinawafikia, asije akafikiri hili lililotokea kwa Sheikh Ponda ni suluhisho, ni vyema kufanya mazungumzo ili kuweka mabadiliko.

Alivyowaponyoka polisi
Mtu wa karibu wa Sheikh Ponda alisimulia jinsi walivyomsafisha kiongozi huyo kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na kukwepa vizuizi vya polisi ambao walikuwa wakiendelea kumsaka. “Msafara ulikuwa na magari mawili. Moja lilitumika kwa uangalizi, lingine lilimbeba Sheikh Ponda. Tulipofika Chalinze tulikuta kizuizi tukakikwepa kwa kupitia Msata kisha Bagamoyo hadi Dar es Salaam na kumfikisha Muhimbili,” alisema.
Waigomea polisi
Msemaji wa familia ya Sheikh huyo, Isihaka Rashid alisema hawaitambui tume iliyoundwa na polisi kwa kuwa jeshi hilo ndilo linalotuhumiwa.
“Tunachofanya hivi sasa ni kukusanya ushahidi wetu, kwa bahati nzuri tayari tumepata mkanda wa tukio lenyewe ambao utatuwezesha kumbaini aliyemshambulia Sheikh Ponda.
“Hatuwezi kuhitaji majibu ya hiyo tume yao na hata leo kuna maofisa wa polisi kutoka Makao Makuu na Kituo cha Kati, Dar es Salaam walifika wakitaka kumhoji eti kuhusu uchochezi lakini alikataa kuzungumza hadi mwanasheria wake awepo, wakaondoka,” alisema Rashid.

No comments:

Post a Comment