Monday, August 12, 2013

SHEIKH YUSUFU MUSSA KUNDECHA AIPA SHARTI SEREKALI YA TANGANYIKA


Sheikh Kundecha atoa sharti
Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini Tanganyika, imeitaka Serikali kuunda tume huru ya uchunguzi wa tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na majibu yake ndiyo yatakayoamua uhusiano baina ya Waislamu nchini na Serikali mfu iliyopo madarakani.
Akitoa tamko la Jumuiya hiyo katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, Dar es Salaam nchini Tanganyika jana, Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh Yusufu Mussa Kundecha alisema pamoja na mambo mengine, pia wanataka kuona askari polisi aliyemdhuru Sheikh Ponda anachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda ni mtiririko wa vitendo vya uonevu na unyanyasaji na aliishangaa Serikali kumtafuta Sheikh huyo kupitia vyombo vya habari wakati inafahamu hatua za kuchukua pale wanapokuwa wanamtafuta mtu.
Alisema hata yeye wakati anatafutwa na polisi alipelekewa barua akitakiwa kuripoti kituoni lakini si kupitia vyombo vya habari na kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa Serikali imeshindwa kuwahakikishia raia usalama wao.
“Bayaa zaidi, wao ambao wanataka watu wasichukue sheria mkononi ndiyo hao wa kwanza kufanya hivyo jambo ambalo sidhani kama litatufikisha pazuri,” alisema Sheikh Kundecha.
Aliitaka Serikali kufuata sheria na kufuata taratibu husika katika kushughulikia masuala yanayowahusu makundi mbalimbali katika jamii badala ya inavyofanya sasa akisema hiyo inachangia chuki kati ya Waislamu na Serikali.
Nae Profesa Lipumba atoa tamko
Mwenyekiti wa (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati suala la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda ili nchi isije kuingia kwenye machafuko yenye mrengo wa kidini.
Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake Dar es Salaam kuwa chama hicho kinalaani vikali tukio hilo na kutaka polisi kuwakamata waliompiga risasi.
“Nimetoka kumjulia hali muda mfupi uliopita, nimemkuta akiwa katika hali mbaya japo anaweza kuzungumza na kutambua watu wanaokwenda kumwona… kwa kweli tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda linaweza kusababisha nchi kuingia kwenye machafuko ya kidini kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Tukio la Sheikh Ponda kupigwa risasi tena na watu wanaodhaniwa kuwa ni polisi, limeleta sura mbaya kwa taifa,” alisema Lipumba.
Rufaa ya wafuasi wake leo
Wakati hayo yakitokea, rufaa ya wafuasi 52 wa Sheikh Ponda waliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Wafuasi hao walihukumiwa kifungo hicho, Machi 21, mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, kutenda makosa, kukaidi amri ya polisi kabla na baada ya kufanya maandamano yaliyozuiwa na polisi, kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi yote haya yakiwa ni ya serekali mfu inawapakazia na kuwaenezea ubaya rai wema wenye kutaka mabadiliko.
Hata hivyo, kupitia kwa Wakili wao, Mohamed Tibanyendera walikata rufaa wakipinga hukumu na adhabu waliyopewa.
Rufaa hiyo itasikilizwa leo na Jaji Salvatory Bongole.
Kwa mujibu wa hati ya rufani waliyoiwasilisha mahakamani hapo, wafuasi hao, pamoja na mambo mengine, wanadai kuwa hakimu alikosea kisheria katika kuchambua ushahidi wa pande zote uliowasilishwa mahakamani.
Pia wanadai kuwa katika hukumu hiyo, hakimu alijichanganya kwa kumwachia huru mmoja wa washtakiwa na kuwatia hatiani washtakiwa wengine.
Watu hao walikamatwa na Polisi Machi 15, mwaka huu, wakiandamana kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa lengo la kumshinikiza kumpa dhamana Sheikh Ponda na mshtakiwa mwenzake Mukadam Swalehe na Machi 18, mwaka huu walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka.

No comments:

Post a Comment