Tuesday, September 10, 2013

PELE WA NCHI YA ZANZIBAR MAJHAM NI ALMASI ISIYO THAMINIWA NCHINI MWETU ZANZIBAR

Timu ya Zanzibar kwenye Kombe la Gossage la mwaka 1952.
 

Timu ya Zanzibar kwenye Kombe la Gossage la mwaka 1952.
 
Na Hamza Z. Rijal. WENGI wanamjua kwa jina lake la mkato: Majham. Kuna wanaomwita ‘Pele wa nchi ya  Zanzibar’.  Angelikuwa amezaliwa Ulaya, Marekani au hata Amerika ya Kusini hii leo angelikuwa anaenziwa.  Hakujaaliwa bahati ya akina Boby Charlton, Geoff Hurst, Johan Cruyff, Platini, Pele, Blokhin, Hadji, Latto, Tostao, Gerson, Romario.
Angelijaaliwa bahati hiyo basi angelikuwa fahari ya nchi ya  yake Zanzibar  kwani zama zake Majham alikuwa amebobea katika michezo miwili — soka na hoki (mpira wa magongo).  Viwanja vya soka vikimjua, viwanja vya hoki vikimtambua.
Siku hizi ukimtafuta Majham hutompata kwenye viwanja vya soka wala vya hoki.  Kwanza vya hoki haviko tena ndani ya nchi ya Zanzibar kwani hoki haichezwi tena nchini mwetu.  Mchezo huo ulipigwa marufuku baada ya Mapinduzi ukionekana kuwa ni spoti ya kibwanyenye.
Siku hizi ukimtaka Majham itakubidi wende Mchangani. Zikate kona mbili tatu hadi nyumbani kwake. Ukibahatika utamkuta amekaa barazani. Saa zote anakuwa mpweke hapo barazani kwake akitafuta rubaa la washabiki wa spoti wa kuweza kuzungumza naye. Ingawa ni mpweke hataki kujinasibisha na chochote kile.
Hii leo Majham — jina kamili Abdul Majham Omar — amekuwa mfano wa lulu iliyotupwa. Pamoja na uzee, ana umri wa miaka 79,  Majham siku hizi ni dhaifu, ganzi ya miguu inamsumbua na haoni sawasawa. Mwandishi aligundua kitu kimoja cha ki-Majham pekee: kinapotokea kitu katika mazungumzo kinachomkuna husema ‘awii’.
Mwandishi: Je unakumbuka mwaka uliozaliwa?
Majham: Miye sikumbuki lakini labda uwaulize wale niliocheza nao watu kama kina Sayyid Ali Soud, lakini ninachoweza kukisema kuwa ninafahamu fika kuyajuwa yaliokuwa yanaendelea kwenye Vita Vikuu vya Pili  wakati huo ni mtoto wa makamo naenda chuoni kusoma Qur’an.
Mwandishi: Itakuwa labda una umri wa miaka 9 hivi wakati huo wa Vita Vikuu vya Pili vya dunia?
Majham: Zaidi, labda miaka 11 au 12.
Mwandishi: Nikifanya mahesabu unafikia umri wa miaka 79.
Majham: Nakubaliana na wewe.
Mwandishi: Nielezee maisha yako kwa mukhtasar?
Majham: Mimi ni mzaliwa wa mtaa wa Malindi na ndipo nilipokulia. Nalianza masomo yangu ya Qur’an chuo cha Maalim Jeledi.  Nilisoma hapo mpaka nikahitimu na huku nikiendelea na masomo ya msingi katika skuli ya Gulioni.  Naikumbuka Gulioni na nina masikitiko kuwa jengo la skuli hiyo halipo. Nawakumbuka baadhi ya walimu wetu ambao walikuwa sio walimu wenye kusomesha lakini walikuwa ni wazazi wetu. Unaposomeshwa na Maalim Burhan au Maalim Buda au Maalim Badi unajikuta kuwa upo na sehemu ya wazazi wako. Sijabahatika kusoma na kufika mbali, nalimaliza masomo hapo Gulioni skuli nilipofika chumba cha 5.
Mwandishi: Baada ya masomo ya msingi ulikuwa unafanya nini?
Majham: Zamani sio leo, kila mtu alikuwa ni mzee.  Nilitafutiwa kazi [na wazee] na kupata kazi sehemu ya Umeme pale Public Works Department (PWD) na nilifanya kazi hapo kwenye miaka ya 1950 hadi kufikia Mapinduzi. Halafu nikawa nafanya kazi katika Shirika la Umeme na nimefanya kazi hapo hadi kufikia kustaafu.
Mwandishi: Baada ya kuzungumzia maisha yako kwa jumla hebu tugeukia michezo. Kitu gani kilikuvutia kucheza soka, hoki (mpira wa magongo) na kriketi (cricket)?
Majham: Nimeanza kucheza soka nikiwa na umri wa miaka sita na nilikuwa hodari wa kupiga chenga tangu umri huo. Ninapocheza na watoto wenzangu kila mtu huvutiwa namna ninavyochukua mpira na kuwapiga chenga wenzangu. Nilipokuja kuona filamu ya Garincha pale Ofisi ya Filamu ya kina Mohammed Kassim, hapo ndipo ikawa nikichocheo kikubwa kwangu kuwa nakokota mpira na kuhesabu wachezaji, ingawa Mwalimu wetu ‘Mr. Mazal’, huyu ni Ahmed Iddi Mjasiri. alikuwa hapendi kumuona mtu anakaa na mpira kwa muda mrefu.
Mwandishi: Majham wewe ni mzaliwa wa Malindi, verejee ukachezea Vikokotoni?
Majham: Ukweli miye sipendi mambo ya kifahari wala kujiweka mbelembele. Miye mambo yangu ni kutopenda mambo ya kifakhfakh. Kwa sababu hizo ndio nikenda  Vikokotoni, ingawa nilicheza muda mfupi katika timu inayoitwa Hadhrami.  Haya mambo ya Hadhrami yawache kwani yana hikaya refu.
Mwandishi: Kwa nini isiwe Kikwajuni, Mwembeladu, Miembeni?
Majham: Miembeni au Kikwajuni zama hizo kulikuwa ni sawa kwa leo kama upo maeneo ya Mwanakwerekwe,. Doooh, ingekuwa taabu kwangu.
Mwandishi: Taabu ya nini?
Majham: Uwwih, alaaa, [kacheka sana bila ya kutaka kuendeleza].
Mwandishi: Ulianza kuchezea Gossage mwaka gani?
Majham: Nakumbuka nilianza kucheza Gossage 1952 nakupa na hiyo picha uone .  Nilikuwa na kina Mzee Mwinyi(Mpiringo) Mzee Ahmed Islam, Seif Rashid, Maulidi Mohamed (Machaprala) na wengineo. Tulicheza Nairobi tulikuwa washindi wa pili. Tuliwafunga Waganda na Tanganyika, tulilala kwa Kenya na ukweli Kenya ikitupa tabu sana, kwani wakitumia nguvu za hali ya juu na sisi tulikuwa na wachezaji wachache ambao wakitumia nguvu.  Sisi mchezo wetu ni dama, mfano wa Brazili. Unaweka karata kwenye bao, unaanza nyuma unafika kati, unachezewa kidogo, unapelekwa wingi, unawekwa kati, haooo, tunarudi, huo ndio mtindo wetu. Kenya wao pasi tatu wako golini.
Kutoka hapo niliendelea kuchaguliwa kwenye timu ya Gossage mpaka mwaka wa 1968 ndio nikamalizia kucheza timu ya taifa. Nimecheza na kina Kassim bin Mussa, Sururu, Khalid Kessi, Boti mkubwa wa Malindi, nikaja nikacheza na vijana kina Boti mdogo, Abdimout Ajmi, Saad, Hijja Saleh, Seif Rashid, Seif Nassor (Mshumaa).  Kisha nilikuwa na fowad nikistaladha kucheza nao, huku Ahmada Mwanga, huku Mossi Kassim, Mkweche kushoto, Ahmada Mwanga na mfalme wa hewani Mohammed Kassim, uwwih, alaaa. Hapo nakwambia kigoma tukikipiga, waulize Warusi waliokuja na kuzifunga timu zote za Afrika Mashariki na kuja hapa tukenda suluhu nao, Warusi hawajaweza kuamini, siku hiyo mpate Ahmada Mwanga na Mkweche watakuelezea kigoma tulivyokipiga, ilikuwa kila mtu anazungumza juu ya game hii.

Timu ya Zanzibar kwenye Kombe la Gossage la mwaka 1962.

 
 
Timu ya Zanzibar kwenye Kombe la Gossage la mwaka 1962.
 
Mwandishi: Mchezo gani unaoukumbuka na hutousahau?
Majham: Gossage Zanzibar mwaka wa 1966, timu yetu ilikuwa 1. Bobea. 2. Sleiman Amour 3. Tindo 4. Ahmed Himidi London 5. Majham 6. Kitwana Rajab 7. Mossi Kassim, 8.Mohammed Kassim. 9. Peter 10. Ahmada Mwanga 11. Maalim Seif Nassor (Mshumaa). Tulifungwa na Kenya, tukalala kwa Tanganyika na tukenda suluhu na Uganda.  Natamani kungekuwa na filamu yake ungeona namna tunavyocheza. Yule kocha wa Tanganyika aliwahi kusema lau ningeipata timu hii ya Zanzibar ningekuwa juu.
Mwandishi: Tuzungumzie hoki (mpira wa magongo) na kriketi (cricket).
Majham: Kriketi sijacheza. Nilijaribu nikaona mchezo haunifai, kwani unachukua muda mrefu, lakini mpira wa magongo nilicheza baada ya kushauriwa kuwa nitasaidia hoki ambayo ilianza kupotea baada ya Mapinduzi. Nikasema kuwa nipo tayari lakini naogopa kucheza mbele, nikapendekezwa nicheze golikipa na nikakubali. Ukipa wangu ulikuwa nachanganya na utaalamu wa soka nikawa natoa pasi nacheza kijanja, nikapata sifa nikawa nachaguliwa timu ya taifa miye, kijana Islam Ahmed Islam nimecheza mpira na babake, halafu huyu Daktari Mohamed Jidawi tukicheza pamoja timu ya Taifa ya Tanzania.
Umetaja kriketi, nikipenda kuwaangalia vijana wawili wazalendo wakichezea Comorian, Zaghalouli na Ahmed Himidi. Wakikutana hao, basi utaona raha. Zaghalouli anapiga mipau, mipira kaokote jumba la Makumbusho, lakini Ahmed Himidi kutwa yupo kiwanjani anazuia tu, akiwapa taabu kwelikweli warushaji mipira.
Mbona leo umeazimia kutaka kuniliza? Leo wapi… nchi hii watu wakicheza futuboli, hoki, kriketi, tenis hata gofu. Michezo yote imekufa isipokuwa soka. Kuna wachezaji kama Ahmed Himidi London akicheza michezo yote hio, sio kucheza tu, lakini akichaguliwa katika timu ya taifa kwa kwa kile mchezo.
Mwandishi: Una nyongeza?
Majham: Nyongeza ninayo. Kwanza mbona hujaniuliza kuwa timu ya kwanza kucheza kombe la klabu la Afrika ilikuwa ni Cosmopolitan chini ya Mwalimu Mansour Magram. Tulicheza na timu ya Somalia tulikwenda suluhu 1-1 pale kiwanja cha Ilala Dar-es-Salaam na tukashindwa kwenda Somalia kwa mbinu za FAT kutotaka twende. Silisahau hili. Tupo klabu tunasubiri safari na mabegi yetu tunaambiwa hamna safari. Tulikuweko pale kina Abdimout, Msuba, Msomali, Emil Kondo, Marandu, Abuu, Kitwana Douglas, Masiku, Rajabu, Iddi Balozi, Makanda. Tulikuwa tuelekee Somalia zikafanywa hila na haya yanakwenda na kujirejea.
Jengine, kama unavyoniona nipo mgonjwa. Nashukuru nimepata kuonana na Rais [Ali Mohamed Shein] nikaambiwa nitapatiwa matibabu nje ya nchi, lakini hadi leo hakuna lilofanyika na hali yangu ya kiafya inakwenda chini. Aidha namshukuru Waziri Mohammed Aboud na ile kamati ya mtoto wa muuza magazeti [Farouk Karim] na wewe mwandishi naambiwa umo, kufanyisha mchango wakuweza kunisaidia nashukuru sana, sana.
Wito wangu Serikali ijuwe sisi tulilitumikia Taifa basi tuangaliwe kama wenzetu huko Ulaya na kwengineko. Tumetupwa useme kanda la usufi, puuuu!

No comments:

Post a Comment