Thursday, June 12, 2014

HONGERA ASHA BAKARI,BALOZI MDOGO WA TANGANYIKA NA SALMIN AWADHI SALMINI KWA KUWAONYESHA WAZANZIBARI MULIVYO MAHASIDI WA SUK NA WAZANZIBARI KWA UJUMLA



WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesisitiza msimamo wao wa kuwasilisha hoja binafsi ambayo itaamua kama muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) uendelee kutumika au ufutwe kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015.
Shinikizo la kusudio hilo, limeendelea kusisitizwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Viwanja vya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, uliohudhuriwa na wawakilishi wa CCM.
Miongoni mwa wawakilishi ambao walihutubia mkutano huo ni pamoja na Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi, Salmin Awadhi Salmini na Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Katika maelezo yake, Salmini alisema baada ya kuwasilishwa hoja hiyo katika Baraza la Wawakilishi, baadaye ataipeleka kwa wananchi ili waulizwe kama wanataka kuendelea na mfumo huo au la.
Alisema tayari hoja hiyo imeandaliwa na wakati wowote wataipeleka katika Baraza kwani Serikali ya umoja huo ambayo inajumuisha chama tawala cha CCM na Chama cha Wananchi (CUF) ambayo haijaleta manufaa yoyote kwa Zanzibar, tangu kuanzishwa.
“Tangu kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa…hakuna linalofanyika badala yake tunashuhudia matukio ya ajabu ajabu yakiwemo ya vurugu…vifo na watu kuhujumiwa kwa kumwagiwa tindikali,” alisema Salmin.
Salmini ambaye ni mwakilishi wa CCM Magomeni alisema hivi sasa, CUF hawana amani tena baada ya kusikia CCM inataka kupeleka hoja hiyo kwenye Baraza kwani kuidhinishwa kwa Serikali hiyo kulitokana na hoja binafsi na wao watapeleka hoja binafsi.
Aliwataka viongozi wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUWAMAZA) kuacha kuchanganya dini na siasa kwani kufanya hivyo ni kutaka kuanzisha vurugu na kuhatarisha amani na utulivu ndani ya nchi.
Aliongeza, viongozi hao wanastaajabisha sana kwa kupeleka barua kwa Rais, wakimtaka asikubali kusaini hoja hiyo wakidai Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyopo, ina amani na utulivu.
“Leo kwa kuwa tunataka kupeleka hoja binafsi ya kutaka kuvunjwa Serikali hii…JUWAMAZA wana wasilisha barua kwa Rais…haya matukio yote ambayo yametokea ya kujeruhiwa na kuuliwa viongozi wa dini ya Kikristo pamoja kumwagiwa tindikali viongozi mbalimbali wa dini hawakuyaona…sasa walikuwa wapi…mbona hawakutuma barua,” alihoji Salmini.
Naye Mwakilishi wa Viti Maalumu, Asha Bakari Makame alisema wameamua kupeleka hoja hiyo kwa sababu Serikali ya Umoja wa kitaifa haina maana na uwezo wa kuiondoa wanao .
Kwa upande wake, Balozi Seif Ali Iddi aliwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) waliotoka nje ya Bunge Maalumu la Katiba warudi bungeni, ili wajumuike na wenzao kujadili na kutetea muundo wa Muungano wanaoutaka kwa kujenga hoja.
Alisema CCM hawabadiliki na hawatarudi nyuma bali wataendelea kutetea muundo wa Muungano wa Serikali mbili kama katiba ya CCM inavyoeleza. Hivyo ni vyema warudi bungeni kutetea muundo wanaoutaka na wao watetee muundo wao badala ya kutafuta visingizio.
“Kitendo walichokifanya UKAWA kutoka nje ya Bunge na kuanza kupita mitaani hakiwasaidii kwani Katiba ya nchi haitungwi mitaani wala katika mikutano ya hadhara inatungwa katika Bunge ambalo ni chombo kilichowekwa maalumu kufanya kazi hiyo,” alisema na kuongeza:
“Nawaomba vijana msikubali kushawishiwa na kuingia katika mambo ambayo hayataleta manufaa kwenu bali yatawaingiza katika vurugu na kuvunja amani na utulivu uliopo ndani ya nchi,” alisema Balozi Seif.
Alisisitiza kuwa lazima vijana wawe macho na watu wa aina hiyo kwa sababu wanataka kuwaletea vurugu ndani ya nchi sambamba na kuwataka wanawake kuwaunga mkono katika Uchaguzi Mkuu 2015 kwani wanawake ndio nguzo kuu wanayoitegemea kukiletea ushindi chama hicho.

No comments:

Post a Comment