Wednesday, June 25, 2014

MALI ZA MBUNGE MOJA WA NCHI YA TANGANYIKA KUPIGWA MNADA (itabidi acheze mnanda sasa) NDIO MAANA WANAJIDA SEREKALI TATU ZINA GHARAMA KUMBE MAJIZI MAKUBWA YANAWANYONYA TU RAI

bbh
Kapteni John Komba
Waziri Mkuu Pinda aingilia bila mafanikio
ZIMESALIA siku tano tu, kuanzia Jumatano wiki hii, kabla ya baadhi ya mali za Mbunge maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kapteni John Komba, kupigwa mnada ili kufidia deni kubwa alilonalo katika Benki ya CRDB.
Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zilizopatikana, Komba anayemiliki shule kadhaa jijini Dar es Salaam, ikiwamo ya Bakili Muluzi, anadaiwa na Benki ya CRDB zaidi ya Sh bilioni moja, ikiwa ni deni la msingi pamoja na riba ya asilimia 17 katika miaka mitano anayodaiwa kushindwa kulipa deni hilo.
Deni la msingi ni Sh milioni 900, lililotolewa katika mikupuo miwili; kwanza Sh milioni 300 na baadaye Sh milioni 600, baada ya maombi ya mkopo aliyoyatuma CRDB mwaka 2007, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa madarasa, nyumba za wafanyakazi, mabweni, uchimbaji wa visima na ununuzi wa samani kwa ajili ya madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule yake hiyo ya Bakili Muluzi.
Marejesho ya mkopo huo uliopaswa kulipwa ndani ya miaka mitano, yalitakiwa kufanyika katika mikupuo 22 na kumalizika Juni 30, 2014.
“Januari 14, 2009, Mbunge huyo alipewa na CRDB mkopo wa jumla ya Sh milioni 900 zilizopaswa kulipwa kwa ‘installments’ (mikupuo) 22 na kukamilika Juni 30, 2014,” alisema mtoa habari wetu ambaye ni wazi jina lake hatuwezi kuliweka gazetini kwa sasa.
Katika makubaliano hayo, mbunge huyo kupitia taasisi isiyo ya kiserikali (NGO) anayoimiliki, alipewa ‘grace period’ (kipindi cha muda wa matazamio) wa miezi sita, lakini hata alipoanza kulipa, malipo yake hayakwenda kama ilivyotarajiwa.
“Dhamana ya mkopo huo iliyowekwa benki ni hati tatu za viwanja anavyovimiliki namba 121244 (Plot No, 167/1 Block 1), namba 121245 (Plot No 167/2 Block 1 na namba 55920 (Plot No 1030) vyote vipo Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam,” alisema mtoa habari wetu huku nyaraka kadhaa zikithibitisha.
Uchunguzi zaidi wa Rulibaini kuwapo kwa jitihada za dhati za Mbunge huyo kulilipa deni lake hilo, lakini hadi Aprili 16, mwaka jana, alikuwa amelipa malimbikizo ya deni ya Sh 214,126,678 ambapo Sh 146,126,678 zililipwa katika Akaunti ya Benki ya CRDB, Lumumba namba 01J1008525300.
Fedha nyingine kati ya hizo ambazo ni Sh 68,000,000 zililipwa kwa Mbunge huyo na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanganyika (TACAIDS) katika akaunti yake iliyopo CRDB Tawi la Kijitonyama, jijini Dar es Salaam na kisha yeye mwenyewe akazihamishia Tawi la CRDB Lumumba.
Muandishi wetu halikuweza kufahamu mara moja sababu za TACAIDS kumlipa Mbunge huyo kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Kutokana na kuchelewa kulipa deni katika mtiririko waliokubaliana, hadi Novemba 2011, miaka miwili tu tangu apewe mkopo huo, deni hilo liliongezeka na kufikia Sh 1,252,110,349.14, kitendo kilichosababisha Benki ya CRDB kutafuta dalali wa Mahakama na kumtaka akamate mali za mbunge huyo na kuzipiga mnada wa hadhara.
Dalali huyo, Bani Investment Limited, alipewa kazi hiyo Februari 8 mwaka jana, lakini kabla ya kufanya hivyo, Mbunge alikimbilia Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuweka pingamizi, ingawa tayari wanafunzi kadhaa wa shule anazozimiliki walilazimika kuhamia shule nyingine kutokana na kutofahamu mustakabali wao.
“Wakati wa mgogoro kati yake na CRDB, Mbunge huyo alikuwa akihaha kuhamisha umiliki wa shule zake, kiasi cha kufikia makubaliano na kampuni ya IKS Tanganyika kuiendesha moja ya shule zake kwa miaka mitano huku ikilipa deni hilo kwa niaba ya Mbunge, lakini suala hilo lilishindikana,” taarifa zaidi zinafafanua.
Baada ya kuona kuwa suala hilo linazidi kuwa gumu kwake, Muandishi wetu akafahamu kwamba, Mbunge huyo ambaye ana uhusiano mzuri na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM na Serikali, aliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu (PMO) kuingilia kati suala hilo na kumshawishi Mkurugenzi wa CRDB, Dk. Charles Kimei, amuongezee muda wa kulipa deni lake.
Aprili 23, 2012, PMO ilimwandikia barua Dk. Kimei ikimshawishi kuangalia uwezekano wa kumwongezea muda wakati huo Serikali inatafuta namna stahiki ya kumsaidia kwa kuzinunua shule zake, lakini CRDB iliendelea na msimamo wake wa kutoongeza muda zaidi.
Machi 21 mwaka jana, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliijibu barua ya Mbunge huyo ya Februari 20 mwaka huo huo ambayo haikuwa na kumbukumbu namba, ikimtaarifu kuwa pamoja na kupokewa kwa barua hiyo, Taarifa zilizokifikia chumba cha habari zilisema kwamba, maombi ya Jiji kununua shule na ardhi anayoimiliki, kwamba yatashughulikiwa na Kamati ya Huduma za Jamii; na hadi sasa hakuna majibu aliyopewa.
Kwa sasa, zikiwa zimesalia siku hizo tano tu kufika Juni 30, 2014 ambayo ni siku ya mwisho wa makubaliano, CRDB imekuwa ikiiomba Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuiruhusu kuuza mali zote za Mbunge huyo kufidia deni lao, lakini Mbunge anadai kuwa thamani ya shule zake na ardhi ipatayo mita za mraba 34,735, ni zaidi ya deni analodaiwa.
Mbunge huyo pamoja na mkurugenzi wa CRDB Dk. Charles Kimei hawakuweza kupatikana hadi tunakwenda mitamboni, simu ya Dk. Kimei ikiita bila majibu wakati simu ya Komba ambaye mwandishi wetu hakuweza kumpata licha ya kumfuatilia bungeni mjini Dodoma ana kwa ana, haikuweza pia kupatikana.

No comments:

Post a Comment