Saturday, April 2, 2016

KINARA WA MAPINDUZI NA ALIYEKUWA KATIBU WA KWANZA WA BARAZA LA MAPINDUZI SALIM RASHID AMTAKA MAALIM SEIF SHARRIF HAMAD NA SHEIN KUKUTANA HARAKA


MMOJA wa vinara walio hai wa Mapinduzi ya mwaka 1964, Salim Rashid, amemtaka Shein kukutana kwa haraka na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, “wakiwa peke yao kwanza” kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa visiwani humo. Katika mazungumzo aliyoyafanywa nyumbani kwake, Mbweni, Unguja mwishoni mwa wiki iliyopita, Salim Rashid ambaye alikuwa Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 aliuita Uchaguzi wa Marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu kuwa ni “kichekesho”. Alisema hatma ya Zanzibar iko mikononi mwa Shein na Maalim Seif na kwamba hakuna namna nyingine ya kuvikwamua visiwa hivyo kutoka vilipo sasa zaidi ya kuzungumza. “ Zanzibar imepita katika misiba mingi, fadhaa na machungu tangu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Hakuna maelezo ya kutetea kwamba kwanini Wazanzibari waishi katika hali hii. “ Ni lazima Shein na Maalim Seif wakutane haraka iwezekanavyo na tena wakiwa peke yao kwanza. Wasimhusishe mtu mwingine. Hakuna la Zanzibar wasilolijua.Wakae chini wazungumze na kuelewana. “Zanzibar hakuna chama cha kushinda kwa asilimia 91.4. Kama chama hicho kipo, kwanini hakikushinda kwa idadi hiyo kwenye uchaguzi uliofutwa wa Oktoba mwaka jana..??
“Ule uchaguzi kwa kweli ulikuwa ni kichekesho. Hakuna uchaguzi pale. Takribani nusu ya wananchi walisusa na hawakupiga kura. Sasa ni kiongozi gani anayeweza kupuuza nusu ya wananchi wake...?? Siku hizi, hata asilimia tano tu ya watu ni wengi, sembuse nusu nzima...??” Alihoji. Salim Rashid ambaye ni msomi wa masuala ya uchumi kutoka katika Chuo Kikuu maarufu duniani cha London School of Economics (LSE), sasa ana umri wa miaka 75 lakini bado anaonekana kuwa na nguvu. Alisema kwa watu walioshiriki katika kutafuta Uhuru wa Mzanzibari na hatimaye kuupata, inaumiza sana kuona Zanzibar ilipo leo; tofauti na ndoto zao wakati wa Mapinduzi zaidi ya miaka 50 iliyopita. “Zanzibar ilikuwa maarufu babu. Kulikuwa na mwimbaji maarufu wa hapa akiitwa Sitti binti Saadi aliimba wimbo maarufu akisema; ‘Zanzibar ni njema, atakaye aje’. Wengine wanaopiga kelele leo walikuwa hawajazaliwa wakati huo. “Zanzibar si nchi ya wananchi wake kukosa elimu, ajira na matibabu. Ni lazima viongozi wakae na kuelewana na waweke maslahi ya watu wao mbele,” alisema. Katika mazungumzo yake hayo, mzee Salim Rashid ambaye aliwahi pia kuwa balozi wa nchi ya Tanganyika ((Tanzania)) katika nchi za Guinea na Ethiopia, alimpongeza Maalim Seif kwa utulivu aliounyesha katika wakati huu. Alimtaka Maalim Seif, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi uliofutwa, kuendelea kuwa mvumilivu na mtulivu na kwamba hiyo ndiyo namna pekee ya kurejesha utulivu Zanzibar.
Balozi huyo mstaafu ni mmoja wa wajumbe wanne walio hai wa Baraza la kwanza la Mapinduzi la nchi ya Zanzibar; wengine wakiwa ni Hassan Nassor Moyo, Khamis Ameir, Ramadhani Haji na Aboud Jumbe Mwinyi. Alisema Zanzibar kuna matatizo mengi ambayo yanahitaji mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu na kwamba kadri yanavyochelewa kutatuliwa, ndivyo yanavyozidi kukomaa. “ Kwa mfano, imeonekana kwamba tangu mwaka 1957, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeshindwa kusimamia uchaguzi. Mimi nadhani Wazanzibari wakubaliane kuwa chaguzi zao ziwe zinasimamiwa na Umoja wa Mataifa. “Kama wakikubaliana kwenye hilo, wao hawatakuwa wa kwanza kusimamiwa. Umoja wa Mataifa umewahi kusimamia chaguzi katika nchi za Kosovo, Timor ya Mashariki na kwingineko. Sasa kama mtindo wa kutumia ZEC kila siku unatuvuruga, kwanini tuendelee nao....??” alihoji. Mwasisi huyu alikosoa tabia ya wanasiasa kuendekeza vyama vyao badala ya maslahi ya taifa kwa maelezo kwamba jambo hilo ndilo ambalo limeziangusha nchi nyingi za Kiafrika. Ngoja nikuulize, unajua maana ya chama cha siasa....?? Chama cha siasa kazi yake kubwa ni kushiriki kwenye uchaguzi. Mara baada ya uchaguzi kumalizika, chama cha siasa hakina kazi tena. “ Ndiyo maana unaona kuna wakati Obama alimteua mtu wa Republican kuwa Waziri wa Ulinzi. Sisi hapa Zanzibar tuliamua kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya uchaguzi ambayo inaundwa na vyama tofauti. “Hiyo maana yake ilikuwa kwamba uchaguzi umeisha na vyama vikae pembeni. Sasa watu hawajui hayo mambo. Utasikia mimi CCM, mimi CUF… Vyama ni kitu gani mbele ya maslahi ya taifa.....??

No comments:

Post a Comment